Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri
Polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora wanamshikilia Mwalimu Edward
Kashuma anayefundisha shule ya msingi Simbo, kwa tuhuma ya kumpa mimba
mwanafunzi mwenye umri wa miaka 15 wa anayesoma kidato cha kwanza katika
shule ya sekondari Simbo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Kamanda wa
Polisi mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi, Hamisi Issa, alithibitisha
kukamatwa kwa mwalimu huyo ambapo alidai upelelezi utakapokamilika
mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.
Kutokana na tukio hilo, Issa amewaonya walimu na wananchi kuacha
tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi na kukatisha masomo yao kwani
kufanya hivyo ni kosa la jinai na ni kosa la ubakaji kwani wanafunzi
wengi wako chini ya miaka 18.
Hata hivyo akizungumza kwa uchungu babu na mwanafunzi huyo Luteni
Kanali mstaafu Thadeo Mgoso aliliambia gazeti hili kuwa yeye aliporudi
nyumbani toka Dar es Salaam kuja kuhani msiba alikuta mjukuu wake haendi
shuleni na alipomuuliza dada yake ambaye hakuweza kumtaja jina
aliambiwa kuwa amefukuzwa shuleni kwa ajili ya ujauzito.
Baada ya majibu toka kwa dada yake aliamua kwenda shuleni kuonana na
mwalimu mkuu wa shule hiyo ili kujua juu ya mjukuu wake kukatazwa kwenda
shuleni hata hivyo aliambiwa mjukuu wake ni mjamzito na alipomuuliza
mwanafunzi huyo alidai kuwa alipewa mimba hiyo na Mwalimu Edward
Kashuma.
Kufuatia hali hiyo Mgoso alikwenda Kituo kidogo cha Polisi kutoa
taarifa ili mwalimu aweze kukamatwa ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi
Simbo, David Lukumay alimwambia atampigia simu ili aweze kuja kituoni
lakini pamoja na kukaa muda mrefu kituoni hakuweza kufika.
“Kwa kweli huyo mkuu wa kituo ni mtu wa ajabu mpaka naondoka kituoni
mshtakiwa hakuweza kufika pamoja na kupigiwa simu alisema babu wa
mwanafunzi huyo. Sambamba na hayo Luteni Kanali Mgoso alibainisha kuwa
kilichomshangaza yeye ni maelekezo aliyompa mkuu wa kituo, mtuhumiwa ya
kutaka waelewane kwa kile alichodai mwalimu kuwa endapo atamfikisha
kwenye vyombo vya sheria anaweza kufukuzwa kazi.
Babu huyo wa mwanafunzi alidai mwalimu huyo alifika nyumbani kwake
akiomba waelewane na alipoulizwa juu ya mimba Mwalimu Edward Kashuma
alikiri kufanya mapenzi na mwanafunzi huku akidai yeye alitembea naye
mara moja mwaka jana mwezi wa kumi.
Aidha baada ya hali hiyo babu huyo alipiga simu Polisi tena na ndipo
askari wawili walimfuata mtuhumiwa na kumuweka lupango ambapo amesema
kesi hiyo atahakikisha anaifuatilia hadi mwisho pamoja na mkuu huyo wa
kituo kutaka kuharibu kesi hiyo.
Naye Kaimu Mtendaji wa Kata ya Simbo, Felician Musiba amekiri mwalimu
kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kumpa mimba mwanafunzi wa
kidato cha kwanza ambapo amewataka walimu kuacha tabia hiyo na badala
yake wazingatie maadili ya kazi na kuacha vitendo vya kuidhalilisha
taaluma ya ualimu.