Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Graifton Mushi
MKAZI wa kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga Rehema Tumbo (32) ameuawa na mumewe ambaye alitumia khanga kumnyongwa kwa kile kinachodaiwa alichelewa kurudi nyumbani.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Graiftoni Mushi, alisema mtuhumiwa, Raphael Kazembe anasakwa na Polisi kwani baada ya kufanya mauaji hayo, juzi saa 5 usiku, alikimbia.
Mushi ambaye alithibitisha kuwapo tukio hilo, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo. Mashuhuda wanadai mwanamke huyo baada ya kurudi nyumbani kwake alikuta mlango umefungwa kwa ndani huku mumewe akimsubiri.
Ilielezwa kwamba, alipogonga hakufunguliwa na hivyo alikwenda kulala kwenye chumba cha watoto ambako mumewe alimfuata na kuanza kumpiga hadi kumsababishia kifo.
Mtoto wa marehemu mwenye umri wa miaka 15, alisema mama yake alikuwa amesindikiza wageni na aliporudi nyumbani ndipo ugomvi ulianza kati yake na baba yake.
“Baada ya mama kuona baba hafungui mlango mama alitugongea sisi tukamfungulia ili aje kulala kwenye chumba chetu lakini baba alimfuata na kumpeleka chumbani kwake na kuanza kumpiga na baada ya kuona mama anazidi kupigwa huku akikoroma nikakimbia kwa mwenyekiti kutoa taarifa,” alisema Rafaeli.
Mwenyekiti wa mtaa huo wa Ndala, Edward Mihayo alisema baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka kwa mtoto alifika eneo la tukio na kumkuta mwanamke huyo amelala chini huku akiwa na khanga shingoni akiwa amekufa.

 
Top