WAKATI kesho Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) ikitarajiwa kutimiza azma yake ya kuzima simu ‘feki’ za mkononi, upo
mtikisiko na kizaazaa miongoni mwa watumiaji wa vifaa hivyo vya mawasiliano,
wakisaka mbadala na wengine wakisubiri kuona kama ‘yatatimia’.
Ingawa uzimaji wa simu bandia na kuanza
kutumika kwa teknolojia mpya ya simu za mkononi kwa Mfumo wa Rajisi,
unatarajiwa kuwa muarobaini wa wizi kwa simu za mkononi na kiama kwa
watukanaji, watumaji picha chafu, baadhi ya wanajamii wanaipokea hatua hiyo kwa
mtazamo hasi, wakiangalia hasara watakayopata baada ya simu zao kufungiwa.
Kizaazaa kimekumba siyo tu watumiaji wa simu,
hususan wale ambao wameshabaini kuwa simu zao ni bandia, bali pia wenye maduka
ya simu ambao baadhi inadaiwa kusafirisha simu hizo kwenda kuziuza nchi jirani.
Wakati hayo yakijiri miongoni mwa watumiaji wa
simu za mkononi, kwa upande wao, kampuni za simu za mkononi zimetumia fursa
hiyo kufanya biashara ya simu za mkononi kwa bei nafuu, itakayowezesha wenye
kipato cha chini kumudu bei yake.
Watamani siku ifike
Baadhi ya wafanyabiashara wa simu jijini Dar
es Salaam waliozungumza na gazeti hili, walieleza matamanio yao ya kuzimwa simu
bandia ili biashara yao iendelee, kwa kile walichosema imedorora tangu TCRA
ilipotangaza uamuzi wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana,
walisema kumekuwa na hofu miongoni mwa wateja ambao wengi wanachelea kununua
simu kutokana na hofu ya kuuziwa zilizo bandia.
“Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, biashara ya
simu imeyumba kwa kiasi kikubwa kutokana na tangazo la TCRA,” alisema Mohammed
Bakari ambaye hata hivyo alisema binafsi anauza simu halali, ambazo pia
zimekosa soko kama ilivyo kawaida kutokana na kuhofia za bandia.
Mfanyabiashara mwingine, Erick Ngamwe alisema,
uamuzi wa serikali wa kuzima simu hizo ni jambo zuri. Alishauri isitoe muda wa
ziada ambao kwa mujibu wake, utaendelea kuyumbisha biashara yao.
Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine wa
Kariakoo, Nassor Said alisema, wapo baadhi yao ambao wataumia kwa kuwa walikuwa
na mzigo mkubwa wa bidhaa hiyo.
“Hili tunaliona jambo zuri lakini kuna watu
wanaumia, watu walikopa fedha kuagiza mzigo wa simu leo hii hajamaliza hata
kerejesha pesa yote, simu zinazimwa na anakuwa anapata hasara, kwahiyo si jambo
la kufurahia,” alisema Said.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliohojiwa juu ya
hatua hiyo inayotarajiwa kutekelezwa kesho, waliomba muda uongezwe huku
walilaumu kitendo cha mamlaka zinazohusika kufumbia macho uingizaji wa simu
bandia kuwa ni adhabu kwa watu wenye kipato cha chini.
Wateja wawa makini
Hata hivyo katika maeneo mbalimbali, mwandishi
alishuhudia umakini kwa wanaonunua simu ambao wengi walikuwa wakilazimika
kutumia kanuni iliyotolewa na TCRA, kubaini kama simu anayonunua ni bandia au
halisi.
Wakiwa kwenye gulio la simu lililoandaliwa na
kampuni za simu jijini Dar es Salaam hivi karibuni, walionekana watu wengi
waliokuwa wakinunua simu za gharama nafuu huku wakihoji maswali kuhusu uhalali
wake. Kampuni zatoa ofa Kampuni zinazotoa huduma za simu zimesema zinaendelea
kusambaza simu za gharama nafuu nchini na kutoa ushauri kwa wateja .
Alipohojiwa juu ya athari watakazopata wateja
wenye simu feki baada ya simu zao kuzimwa, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano
na Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosallyn Mworia alisema laini za wateja
hazitaathirika, bali simu bandia wanazotumika ndizo hazitafanya kazi.
Wakati huo huo kampuni ya simu ya Airtel
imetangaza ofa kwa watu wanaohitaji simu halali, kuendana na matakwa ya
serikali ya wananchi wake kutumia simu zinazokubalika kiafya na zenye ufanisi
mkubwa.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana, kampuni
hiyo imesema Airtel Tanzania imeanzisha ofa ya kununua kifurushi chenye thamani
ya Sh 22,000 kupata simu ya bure.
Mkuu wa kitengo cha Intaneti, Gaurav Dhingra
alisema: “Tunatambua kwamba baadhi ya wateja wetu bado wanatumia simu ambazo
hazina uhalisia, hivyo wako katika hatari ya kuzimiwa simu zao hapo itakapofika
siku ya Alhamisi, Juni 16 (kesho).”
Wizi wa simu basi
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa
habari na wafanyabiashara wa maduka ya simu mjini Kigoma jana, Kaimu Meneja wa
Kanda ya Kati wa TCRA, Esuvatie Masinga alisema teknolojia hiyo itasaidia
kudhibiti wizi wa simu za mkononi nchini.
Alisema simu itakayoibwa na kutolewa taarifa,
itafungwa na haitaweza kutumika mahali popote duniani. Alisema teknolojia hiyo
itadhibiti matumizi mbalimbali yasiyofaa ya simu za mkononi, ikiwemo
wanaotukana, wanaotuma picha chafu na matumizi mengine yanayokatazwa.
Masinga alisema simu inapoibwa, utambulisho wa
simu hiyo utaonekana kwenye laini nyingine itakayowekwa iwapo simu hiyo
itaendelea kutumika. Mtu aliyekuwa na simu hiyo, atafuatiliwa na kukamatwa.
Sambamba na hilo, Meneja huyo alisema kuwa
mfumo huo, unatoa faida kwa wanunuzi wa simu, ambao watapaswa kupewa garantii
ya mwaka mmoja ya matumizi, jambo linalowalazimisha wafanyabiashara wanaouza
simu kuuza simu halisi na siyo bandia.
Meneja huyo wa TCRA alisema simu zote na vifaa
vyote vya mawasiliano ambavyo ni bandia, vitazimwa kama ambavyo imeshatangazwa
awali na hakuna muda wa nyongeza kwa simu bandia kuendelea kutumika.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,
Emanuel Maganga alisema udhibiti wa Mfumo wa Rajisi wa Simu za Mkononi,
utasaidia kudhibiti uuzwaji wa simu holela, ambao unachangia kuwafanya
wafanyabiashara kukwepa kukodi.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa alishauri bei za simu
iwe ambayo wananchi wote watamudu. Aliomba mamlaka isimamie hilo, kuhakikisha
linatekelezeka.
Habari hii imeandikwa na Katumba Masamba, Dar
na Fadhil Abdallah, Kigoma