MKUU wa Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Venance Mwamoto, amevamia jukwaa la mkutano wa NCCR-Mageuzi na kisha kumtolea lugha ya matusi Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali.

Mwamoto alijikaribisha kwenye mkutano huo uliokuwa ukihutubiwa na Katibu Mkuu, Mosena Nyambambe kisha akaketi kiti cha mbele walipokuwa viongozi wengine wa chama hicho na kuanza kumchokoza Mkosamali kwa kumtolea lugha chafu kwa sauti ya chini.

Mkuu huyo wa wilaya anadaiwa kufikia hatua hiyo ya kuporomosha matusi kwa kilichoelezwa kuwa alituhumiwa na Mkosamali kwenye mkutano, kwamba amejimilikisha isivyo halali ekari 73 za ardhi katika Kijiji cha Nduta wakati tayari anatumia wanajeshi kuwaondoa wanakijiji hao kwa kile kilichodaiwa ni kutaka kubadili matumizi ya ardhi ili kijiji hicho kiwe hifadhi.

Sokomoko hilo lilimalizwa kwa busara za wabunge, David Kafulila (Kigoma Kusini) na Moses Machali (Kasulu Mjini) baada ya Mwamoto na Mkosamali kukaribia kuzichapa kavu kavu jukwaani.
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia ishara za kutoelewana kati ya viongozi wa NCCR-Mageuzi na mkuu huyo wa wilaya kutokana na kutopendezwa na kitendo chake cha kuvamia mkutano wao.

Mara baada ya Nyambambe kumaliza hotuba yake, Mkosamali wakati akijibu maswali ya wananchi ndipo alitoboa siri ya zogo lililokuwa limetokea, akisema Mwamoto alimvamia jukwaani na kumwambia maneno machafu.

Kwamba Mwamoto alimwambia kuwa wananchi wa Kijiji cha Nduta anaowapigania watahama kwa kutumia nguvu za kijeshi.

“DC amekuja hapa jukwaani, ameniambia maneno mabaya sijafurahia, amezungumzia hata suala la Kijiji cha Nduta na kusema wataondolewa kwa nguvu wakati anajua suala hilo lipo mahakamani. Yeye na wenzake wanataka kujimilikisha isivyo halali, sasa nitaanza kufanya siasa ninazojua kutokana na alivyonifanyia hapa,” alisema.

Tanzania Daima Jumatano limeona mchoro uliochorwa na Bwana shamba ukionyesha kuwa Mwamoto atamiliki ekari 73.9; maofisa kilimo wa Kibondo ekari 57; Shule ya Sekondari Butirana ekari 20; aliyekuwa Ofisa Maliasili, Zabron Donge ekari 26; Ezekiel Kihuli, Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Kibondo ekari 26; Ofisa Mtendaji, Agness Chuma ekari 3; Ofisa Mtendaji Msaidizi, Alphonsina Madata ekari 3 na Helena Majoro ekari 13.

Huku Mwamoto akizomewa na wananchi jukwaani, Mkosamali alimtuhumu kuwa hajali matatizo ya watu, na kwamba anajifanya kufuatilia usafi wa mji wa Kibondo wakati soko halina choo na kujimilikisha ardhi ya wananchi.

Alipohojiwa na gazeti hili sababu ya kuvamia mkutano huo na kudaiwa kumtusi mbunge, Mwamoto alijibu kuwa haukuwa wa NCCR-Mageuzi bali wa mbunge wa Muhambwe ndiyo maana alikuja bila kualikwa.

Licha ya Mwamoto kudai mkutano huo ulikuwa wa mbunge wa Muhambwe, gazeti hili limeona barua ya polisi ya kuruhusu mkutano huo ambao uliombwa na Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi.
Katibu mkuu huyo, aliaani kitendo cha Mwamoto kufanya fujo kwenye mkutano wake, akisema ni matumizi mabaya ya madaraka ambayo wakuu wa wilaya wamekuwa wakifanya kwa Watanzania.
 



 
Top