Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (kushoto) akifuta machozi huku
akiwa ameshika fomu za kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Bazara la Wanawake wa
Chadema (Bawacha) alizokabidhiwa na baadhi ya wanakwake makao makuu ya Chama
hicho jijini Dar es Salaam jana.
Kufuatia viongozi wa baraza la Wanawake wa Chadema
kujitokeza kwa wingi katika kinyang’anyiro cha kuwania uwenyekiti wa Baraza hilo
(BAWACHA) nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Suzan Lymo.
Wanachama hao wanaowania nafasi hiyo ni pamoja na Mbunge wa
viti maalumu, Chiku Abwao pamoja na Lilian Wasira na Sophia Mwakagenda ambao
wao tayari wamekwisha kurejesha fomu zao.
Kufuatia hali hiyo wanawake zaidi ya 30 kutokea Kinondoni,
Kawe, Pwani, na Ubungo wamejitokeza siku ya jana majira ya saa tano za asubuhi
katika ofisi za Bwawacha na kumchukulia fomu mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
Walipotoka katika ofisi hizo za Bwawacha walianza safari ya
kumsaka mheshimiwa huyo ili kumkabidhi fomu hiyo. Msafara huwo wa kumsaka
Halima Mdee uliokuwa ukiongozwa na mwenyekiti wa wazee kata ya Kunduchi,
Elefidena Mali ulikwenda moja kwamoja hadi kwenye ofisi za makao makuu ya
Chadema na kufanikiwa kumkuta mheshimiwa huyo.
Walimuomba mbunge huyo kupokea fomu hiyo, na Halima
Mdee alikubali kupokea fomu hiyo huku akibubujikwa na machozi. Alitoa shukurani
zake na kuwaomba wampe nafasi ya kulifikiria jambo hilo kwa makini halafu
atawafahamisha kile ambacho atakifikiria.
Wanawake hao walichangishana pesa kiasi cha shilingi 53,000/
na kumkabidhi mheshimiwa huyo kwaajili ya kulipia gharama za kurejesha fomu hiyo. Ambapo mwisho ni tarehe 30 ya mwezi Agosti.