Straika wa Simba Emmanuel Okwi ambaye anaichezea timu hiyo baada ya kuikana klabu ya Yanga ambayo alikuwa amesaini nayo mkataba, ameonekana kuwa na wakati mgumu wakati anapoitumikia timu yake hiyo ya Msimbazi.

Hali hiyo amekumbana nayo mchezaji huyo katika mechi ya kirafiki iliyochezwa siku ya Jumamosi baina ya klabu hiyo ya Msimbazi na Gor Mahiya ambapo klabu ya Simba iliibuka kidedea kwa mabao 3 – 0.

Kila alipokuwa akigusa mpira Starika huyo alikabiliwa na makelele kutoka kwa mashabiki wa Yanga waliokuwa wakimzomea na kumuita Mwizi, wakimaanisha kuwa ameiba pesa za Yanga kwa kusaini mkataba na kuukana.

Hali hiyo ilionekana kutishia amani kwa kiwango cha mchezaji huyo huku watu wakiamini kuwa anaweza kukata tamaa  na kujikuta akipoteza uwezo wake wa awali katika kulisakata kabumbu.

Hata hivyo Emmanuel Okwi hakuonesha kujali makelele ya mashabiki hao wa Yanga na badala yake kila alipokuwa akizomewa yeye aliwaonesha dole mashabiki wa Simba, ambao walimshangilia kwa nguvu jambo ambalo lilionekana kumpa nguvu na kufanya vizuri.

“Mimi ni mchezaji mkubwa najielewa na ninajiamini vizuri sana. Kelele zao haziwezi kunibabaisha hata kidogo, zaidi nitazidi kufanya vizuri zaidi na zaidi. Kama wanabisha basi wasubiri wenyewe wataona” alisema Emmanuel Okwi
 
Top