Msanii wa muziki wa Hiphop nchini Rashid Makwiro maarufu
‘Chid Benz’, jana alasiri alikamatwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege
wa kimataifa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa
Polisi wa Viwanja vya Ndege, ACP Hamis Selemani, alithibitisha kukamatwa
kwa Chid Benz na kwamba bado anaendelea kushikiliwa na polisi.
“Msanii huyu tumemkamata hapa airport akijaribu kuvuka na
dawa za kulevya kinyume cha sheria akielekea jijini Mbeya. Alikuwa katika
hatua za ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege ya Fastjet kuelekea Mbeya akiwa na
wenzake,” alisema.
Akivitaja vitu alivyokamatwa navyo, ACP Selemani alisema
msanii huyu amekutwa na kete 14 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na mpaka
sasa bado wanaendelea uchunguzi kubaini ni aina gani za dawa hizo.
“Mtuhumiwa huyu tumemkamata na kete 14 pamoja na misokoto
miwili ya bangi, ambayo alikuwa ameiweka katika mfuko wa shati alilokuwa
amevaa. Aidha, tumemkuta na kigae kidogo cha chungu pamoja na kijiko, vitu vya
maandalizi ya kutumia dawa hizo na hivi vyote vimekutwa katika begi lake,”
alisema.
Chid Benz akiwa studio akifanya kazi zake
Alisema hivi sasa msanii huyo anashikiliwa na Jeshi la
Polisi kwa mahojiano zaidi, “Bado tunaendelea kumshikilia na tutahakikisha
sheria inafuatwa kama inavyokuwa kwa watuhumiwa wengine wanapokamatwa na vitu
kama hivi,” alisema kamanda huyo.
Msanii huyo alikuwa anakwenda jijini Mbeya, kwa ajili
ya kushiriki onyesho la ‘Instagram Party’ linalotarajiwa kufanyika leo jijini
humo.
Chidi Benz alikuwa ameongozana na msanii mwenzake Nurdin
Bilal maarufu ‘Shetta’, baada ya kukamatwa na polisi, Shetta aliendelea na
ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege kuelekea Mbeya.
Julai mwaka jana wasanii wawili Melisa Edward na mwenzake
Agnes Gerald ‘Masogange’ walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Oriver Tambo nchini Afrika Kusini, wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal
Methamphetamine takriban kilo 150, zilizokuwa na thamani ya Sh6.8 bilioni.
Chanzo: MWANANCHI