Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Ferdinand Mtui,
Askari nane wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Kigona wakituhumiwa kwa mauaji ya Erick Nilamewa (16) waliyemtuhumu kuwaibia simu moja aina ya Techno na Sh. 6,000.
Tukio hilo lilitokea juzi jioni Mtaa wa Mabatini Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Wanajeshi hao wakiwa nane, walionekana wakimpiga Nilamewa kwa mateke, fimbo na kumchoma na pasi tumboni, kifuani na mgongoni, baada ya kumkamata wakimtuhumu kwa wizi huo.
Mwili wa kijana huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni.
Aidha, Ahamad Mussa, mkazi wa Mabatini eneo la Mwanga Manispaa ya Kigoma/Ujiji, amelazwa wodi namba 7 katika hospitali ya Mkoa Maweni kwa matibabu, kutokana na purukushani hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Ferdinard Mtui, alithibitisha kukamatwa kwa askari hao nane wa JWTZ kwa tuhuma za mauaji ya kijana huyo na kumjeruhi Mussa (16).
Mtui alisema “Ni kweli tunawashikilia wanajeshi nane na tunaendelea na upelelezi, na baada ya uchunguzi tutawapeleka mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.”
Akizungumza na Nipashe kutoka kitandani alikolazwa, Mussa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kitwe, alitumiwa ujumbe wa simu na wanajeshi hao akiwa shuleni ambao walisema kwamba wanamhitaji.
“Baada ya kutumiwa ujumbe huo mimi nilimbipu, akanipigia na kujitambulisha kuwa yeye ni afande Aberi, akasema njoo mara moja nakuhitaji," alisema Mussa.
"Kwa sababu tunakaa mtaa mmoja, pia huwa naingiaga kwenye makazi yao wanaponituma vitu mbalimbali kama sigara, sikuwa na wasiwasi wowote kuhusu wito huo.”
Alisema alipofika alibisha hodi na walimwitikia na kumwambia akae uani ndipo baada ya muda alitoka Aberi akiwa amevaa kaptura ambaye alianza kuita wenzake ambao walianza kumsulubu.
“Nilimsikia akiwaita wenzake wakina afande Mayowa, Ally na wengine nimesahau majina yao lakini jumla walikuwa wanajeshi nane ambao walikuwa wakinipiga.
"Waliniambia ninyooshe miguu yangu juu ya ukuta na niliponyoosha walinipiga na ubao na fimbo ya mianzi kichwani… damu zilianza kutoka.
"Wakachukua maji wakasafisha, wakapiga tena kichwa nikaanguka chini kisha wakanipiga mateke na kunichapa na nyaya za umeme huku wakiuliza ilipo simu na Sh 6,000 nilizoiba,” alisema Mussa.
Alisema wakati hali ikizidi kuwa mbaya, "walichukua chupa ya pombe na kunimiminia" kabla ya kujitokeza mwanamke mmoja wa nyumba ya jirani anayefahamika kwa jina la mama Hoza ambaye aliwaambia wamwache "mtoto wa watu maana watamuua bure.
“Mimi sijaiba simu wala siku ya leo (jana) sijafika kambini hapo.
"Sijaiba wao wakaendelea kunipiga na kunimwagia maji na kunigalagaza kwenye mchanga wakati huo damu zinaendelea kuvuja kichwani, ndipo mimi nikawambia naomba niende nyumbani nikamwambie mama yangu na tulienda na mwanajeshi mmoja na tulipofika nyumbani tulimkuta mama yangu.
"Mwanajeshi huyo akasimama nje mimi nikaingia ndani nikapita uani na kukimbia na ndiyo ikawa pona yangu la sivyo na mimi ningefariki dunia.”
Alisema baada ya yeye kukimbilia ndipo walipomkamata Erick mtaani na kumpeleka kwenye makazi yao ambako walimpiga na kumtesa hadi walipoona hali yake kuwa mbaya, walikwenda polisi kuchukua fomu namba 3 (PF3)kwa ajili ya kumpeleka hospitali ya Maweni kwa matibabu, lakini alifariki dunia.
Mama mzazi wa majeruhi huyo, Mwaisala Ahamad (36) alisema wanajeshi walimuagiza mtoto mmoja kwenda nyumbani kwake kwamba wanamuitaji mtoto wake na aliwaambia kuwa ameende shuleni.
“Waliniomba namba ya simu ya mtoto wangu nikawapatia kwasabababu wanajeshi hawa walikuwa na mazoea na mwanangu," alisema Mwaisala.
"Nilipowapa nilienda kwenye shughuli zangu kama kawaida sikuwa na wasiwasi wowote, hawa tunawajua.
"Wengine wana nyota moja (luteni usu) na wengine mbili (luteni) na wengine tatu (kepteni) na kutokana na vyeo walivyokuwa navyo sikutarajia mtoto wangu yamkute yaliyomkuta.”
Aliongeza kuwa kama askari hao walihisi kuwa mtoto wake ndiye aliyeiba simu yao walipaswa kumkamata na kumpeleka kituo cha polisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mshumbusi Edmond alithibitisha kumpokea marehemu Nilamewa akiwa na majerahe kifuani, tumboni na mgongo lakini akafariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Mwili wake uko chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa Maweni, alisema.