Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga
Mamlaka ya Mapato (TRA), imefanya mabadiliko makubwa baada ya kuwahamisha watumishi wake 104 waliokuwa Mkoa wa Dar es Salaam na kuwapeleka mikoa mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alilieleza Nipashe kwamba watumishi hao 104 wameshahamishwa tangu Februari mwaka huu.
Miongoni mwa watumishi waliohamishwa ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala TRA Makao Makuu, Aboubakar Kunenge, ambaye alihamishiwa mkoani Rukwa, ambako ataendelea na nafasi hiyo ndani ya mkoa huo.
“Ni kweli wafanyakazi hao wamehamishwa, lakini huu ni utaratibu wa kawaida wa kiutawala na tumekuwa tukiufanya kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha utendaji na utawala bora," alisema Kayombo.
"Kila baada ya muda tunawahamisha baadhi ya wafanyakazi wetu.”
Alifafanua kuwa katika uhamisho huo, watumishi 43 wa kituo cha TRA Ilala wamepelekwa mikoa ya Iringa, Kigoma, Mbeya, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Pwani, Tabora, Morogoro, Lindi na Arusha.
Katika kituo cha Kinondoni, alisema Kayombo, zaidi ya watumishi 11 wamehamishiwa kwenda mikoa ya Singida, Iringa, Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Kagera, Mara, Tabora, Arusha na Tanga.
Aidha, alisema katika kituo cha Temeke, watumishi zaidi ya 10 walihamishiwa katika mikoa ya Arusha, Morogoro, Iringa, Tabora, Mara, Kagera, Lindi, Morogoro, Kigoma na Rukwa.
Kwa mujibu wa Kayombo, watumishi wawili kutoka mkoani Iringa wamehamishiwa Dar es Salaam, ambapo mmoja ameziba nafasi kituo cha Kinondoni na mwingine amekwenda Ilala.
Kuna baadhi ya watumishi ambao wakikaa sehemu moja kiutendaji wanajenga mazoea na kujikuta wakifanya kazi kwa taratibu zao na si kufuata sheria ya taasisi au kampuni anayoifanyia, alisema Kayombo.
“Kwa mantiki hiyo, tumeweka utaratibu kwa TRA kila mwaka tunafanya uhamisho ikiwa ni kuwabadilisha watumishi kutoka eneo moja la kazi kwenda jingine, ili kuangalia utendaji kazi wao pamoja na kubaini mambo kadha yanayochangia ufanisi wa kazi.
"Utaratibu huu sio tu TRA, bali unafanywa hata na sekta nyingine za umma na binafsi, mosi ni kuondoa mazoea ya mtumishi na mwajiri wake katika kazi, lakini pia kuhamishwa huko kunaleta mwanga wa kubaini mambo mengi kuhusu mtumishi huyo.”
Mkakati huo wa TRA umekuja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya ghafla na kukuta uozo wa kashfa ya ufisadi wa makontena zaidi ya 300 bandarini yaliyopitishwa bila kulipa kodi na kusababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bil. 80.
Katika kashfa hiyo, Rais John Magufuli alimsimamisha kazi aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, na maofisa wengine wa Mamlaka hiyo waliokuwa madarakani wakati makontena hayo yakitoroshwa.
Maofisa hao pamoja na vibano vingine walitakiwa kutosafiri nje ya nchi na kukabidhi hati zao za kusafiria mpaka pale uchunguzi dhidi yao utakapokamilika.
Wiki iliyopita, Idara ya Uhamiaji nchini, ilifanya mabadiliko ya maofisa wake 14 waandamizi kati ya jumla ya 200 wanaotarajiwa kupanguliwa, kwa kuwahamisha vituo vya kazi kuanzia Ofisi ya Makao Makuu, mikoa, wilaya na mpakani.
Pangapangua ilikuwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alilolitoa kwenye kikao chake na viongozi wakuu wa idara hiyo kilichofanyika Februari 23.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abbas Irovya alisema upanguaji huo unalenga kuimarisha utendaji, ufanisi na dira katika idara hiyo.
“Pamoja na orodha hii ya maofisa waandamizi wanaohama vituo vyao vya sasa kwenda vituo vingine, Idara ya Uhamiaji inaendelea na utaratibu wa kuwabadilisha vituo vya kazi maofisa zaidi ya 200 kutoka sehemu mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri,” alisema.