Alisema kutokana na manispaa hiyo kutokuwa na eneo la wazi, uongozi ulilazimika kutafuta eneo katika Kijiji cha Kising’a, Tarafa ya Isimani linalomilikiwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Uyole.
Iringa. Vijana zaidi ya 1,000 kutoka katika vikundi 36 katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wanatarajiwa kupewa maeneo ya kilimo na Serikali ili kuwainua kiuchumi.

Ofisa Kilimo na Mifugo katika halmashauri hiyo, Robert Semaganga alisema hayo hivi karibuni wakati vijana walipokuwa wakipanda alizeti kwenye mashamba yaliyotolewa na Serikali.

Semaganga alisema mpango huo ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kutaka kila halmashauri kutafuta maeneo ya kilimo kwa vijana.

Alisema kutokana na manispaa hiyo kutokuwa na eneo la wazi, uongozi ulilazimika kutafuta eneo katika Kijiji cha Kising’a, Tarafa ya Isimani linalomilikiwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Uyole.

“Tulipoomba hekta 150 katika kituo hicho, Serikali ya Mkoa ilitoa baraka zote...Lakini manispaa nayo ilitoa kilogramu 500 za mbegu ya alizeti kwa ajili ya kusaidia vijana watakaojitokeza kuunda vikundi,” alisema Semaganga.

Alisema: “Tunamshukuru pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu kwani baada ya kupata shamba na mbegu, amejitolea gharama za kulima. Pia leo ametoa msaada wa usafiri na chakula kwa vijana waliokuja kupanda kwenye shamba hili.

“Mchakato wa kuwapata vijana umeshafanyika kwa kusajili vikundi viwili kutoka kila kata.”

Msambatavangu alisema katika mpango huo ametumia zaidi ya Sh3.5 milioni zikiwa ni gharama za kuandaa shamba la kulima.
 
Top