UTEUZI wa mawaziri na naibu, uliofanywa na Rais John Magufuli kukamilisha Baraza lake la Mawaziri, umepongezwa na watu wa kada tofauti. Watu hao wamesema wanawakubali walioteuliwa huku wakisisitiza wapewe nafasi na muda, waoneshe utendaji wao.
Wasomi, wanasiasa na viongozi wa taasisi mbalimbali, waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walieleza imani waliyonayo kwa mawaziri hao, wakisema chini ya uongozi wa Rais Magufuli, lazima watachapa kazi kwa kuwa Rais ameshaonesha aina ya utendaji anaotaka. Wengine wameguswa na uwapo wa wanataaluma wengi katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano na kusema wanawatarajia kuonesha nafasi yao namna ambavyo wanaweza kuleta mafanikio katika utendaji kazi wao.
Walioteuliwa juzi na wizara zao kwenye mabano ni Profesa Jumanne Maghembe (Waziri wa Maliasili na Utalii), Dk Philip Mpango (Waziri wa Fedha na Mipango) ambaye aliteuliwa kuwa Mbunge. Wengine walioteuliwa kukamilisha idadi ya mawaziri 17 na Naibu mawaziri 14 ni Gerson Lwenge ambaye kitaaluma ni Mhandisi anayekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji; Dk Joyce Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi) ambaye pia aliteuliwa kuwa Mbunge.
Rais Magufuli pia alifanya uhamisho wa Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kwenda Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na kumteua Naibu Waziri mmoja wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi ambaye ni Hamad Masauni. Masauni pia ni Mhandisi. CWT yamkubali Ndalichako Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kupitia kwa Rais wake, Gratian Mukoba, ni miongoni mwa watu waliosifu uteuzi huo hususan kwa kumteua Dk Joyce Ndalichako kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi.
Kiongozi huyo wa walimu, alimwelezea Ndalichako kuwa ni mtu mkweli na mchapa kazi , ambaye wanaamini sekta ya elimu imepata mtu sahihi. “Nampongeza sana Dk Ndalichako kwa kuteuliwa, ni mchapakazi, mkweli na muwazi naamini kabisa sasa elimu imepata mtu sahihi na tuna imani naye na nina hakika tutashirikiana kikamilifu kuboresha mfumo wa elimu nchini,” alisema Mkoba.
Mwanasiasa mkongwe na aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya awamu ya kwanza na tatu, Paul Kimiti, alisifu uteuzi huo na kusema Rais Magufuli amefanya kazi nzuri na makini. “Rais amefanya kazi nzuri, muda alioutumia kutafakari na kufanya uchunguzi wa kina wa mtu anayemteua ni jambo zuri, hakutaka kuteua tu mtu halafu baadaye aje aharibu kazi na kusababisha kubadili baraza katika kipindi kifupi,” alisema Kimiti.
Kimiti alisema Rais amefanya vyema kuangalia watu wachapa kazi. “Tulipe muda baraza lake lifanye kazi na naamini mawaziri watafanya kazi na kuleta maendeleo kulingana na kasi anayoendana nayo rais mwenyewe,” alisema. Kimiti aliwataka mawaziri walioteuliwa kufanya kazi kwa nidhamu ya kweli na bidii bila maigizo kwa kuwa Magufuli, anafanya kwa moyo alioonesha tangu kipindi cha kampeni.
Baraza lipewe muda Mhadhiri katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), Dk Ayub Rioba, alisema ana imani kubwa na mawaziri walioteuliwa huku akisifu uteuzi wa Dk Mpango kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango . “Kwa muda mfupi tumeona kazi nzuri aliyoifanya Dk Mpango alipokuwa Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ni mchapa kazi na kazi yake imeonekana naamini atafanya kazi kubwa,”alisema Dk Rioba.
Akizungumzia juu ya watu wanaoponda uteuzi wa baadhi ya mawaziri katika Baraza hilo, Dk Rioba alisema aina ya uongozi ambao Rais Magufuli anaonesha, ni dhahiri kuwa walio chini yake watafanya kazi hivyo. “Tulipe muda baraza,” alisema Rioba. Pia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo, Anna Mghwira, alipongeza uteuzi wa baraza hilo na kutaka mawaziri wapewe muda wa kufanya kazi.
Mghwira alisema ni vyema serikali sasa ikaandaa mpango kazi wake na ambao utawekwa wazi . Alisema kwa kufanya hivyo, itasaidia katika ufuatiliaji wa yaliyowekwa katika mpango kazi na utekelezaji wake. Mhadhiri wa Mawasiliano ya Umma na Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk Hamza Kondo, alisema uteuzi ni mzuri kwa kuwa Baraza la Mawaziri limesheheni wanataaluma.
“Tuna matumaini makubwa kutoka kwa Dk Philip Mpango na Injinia Gerson Lwenge kwa kuwa watataka kuonesha nafasi ya wanataaluma wanavyoweza kuleta mafanikio katika utendaji kazi,” alisema Dk Kondo. Wakati huo huo, Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam jana, ilieleza kuwa mawaziri hao, wataapishwa Jumatatu.
Wasifu wa Dk Joyce Ndalichako Elimu 1993 – 1997,Chuo Kikuu cha Alberta, Edmonton, Alberta, Canada; Shahada ya Uzamivu (Ph.D) katika Elimu ya Saikolojia ambako alisomea takwimu, vipimo na tathmini.1987 – 1991, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikosemea Shahada ya Kwanza Elimu akijikita kwenye hesabu na elimu.
Uzoefu wa Kazi Aprili 2015 hadi sasa, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, Chuo Kikuu cha Aga Khan katika Taasisi ya Maendeleo ya Elimu , Afrika Mashariki. Septemba 2014 hadi sasa, Profesa Mshiriki katika tathmini, Vipimo na Viwango.
Julai 2005– Agosti 2014, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA). 2000 – 2005, Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Agosti - Oktoba 2005 Mshauri Mkuu Mwelekezi katika mpango wa mapitio ya sekta ya elimu.
Desemba 3 – 31, 2004, Mshauri katika mpango wa kuanzisha mafunzo ya Tehama katika vyuo vya ualimu. Januari 14-25, 2004, Mshauri katika mpango wa tathmini katika elimu msingi. Aprili 5-29, 2004, Mshauri katika mpango wa kutathmini utoaji wa elimu katika kambi za wakimbizi nchini . Septemba hadi Oktoba 2003, Mshauri katika mpango wa tathmini ya elimu kwa wote (EFA).
Machi - Mei 2003, Mshauri wa kuendesha mahitaji ya tathmini kwa elimu isiyo rasmi. Wasifu wa Dk Phillip Mpango Mhadhiri, Kitivo cha Uchumi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) 1988 - 2002 Mchumi Mwandamizi Benki ya Dunia kuanzia 2002 - 2006 Msaidizi wa Rais katika masuala ya Uchumi kuanzia mwaka 2007- 2008 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kuanzia 2009 - 2010 Katibu Mtendaji Tume ya Mipango kuanzia mwaka 2010 -2015 Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kuanzia Novemba 27, 2015 hadi Desemba 23, siku ambayo aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
 
Top