Mbuge wa Morogoro Mjini (CCM) Abdulaziz Abood, amesema atatumia fedha ambazo wabunge wanakopeshwa kununua magari, kuchimba visima vya maji kuwezesha wananchi wapatao 1,700 wa kata ya Mkundi kupata maji safi na salama.
Uamuzi wa fedha za kukopea gari la ubunge , kuelekezwa kutatua huduma za kijamii hasa uchimbaji wa visima vya maji unatokana na kujionea hali halisi ya shida ya maji kwa wakazi hao.
Alisema suala la maendeleo ya wananchi wake lipatewa kipaumbele cha hali ya juu kwa kushiriki moja kwa moja na kwa kutoa misaada ya vifaa na fedha akishirikiana na viongozi wenzake .
Alisisitiza kwamba ataendeleza kasi zaidi ya kuwatumikia wananchi kwa ajili ya kuharakisha maendeleo na upatikanaji wa huduma bora za kijamii zikiwemo za elimu, afya na maji safi na salama.
Alisema katika kutekeleza kaulimbiu ya ‘ Hapa Kazi tu’ , atasaidia upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Mtaa wa Mkundi –CCT , kata ya Mkundi kwa kuchimba visima viwili vya maji.
“Uchimbaji wa kisima kimoja unagharimu zaidi ya Sh milioni 25 na viwili ni zaidi ya Sh milioni 50...hivyo basi nitatumia fedha ambazo wabunge tunapewa kukopeshewa kununua magari yetu , nitazileta zihudumie kwa kuchimba visima vya maji ili mpate maji safi na salama, ” alisema Abood.
Awali, mmoja wa wakazi wa mtaa huo, Nashir Kamugisha , kwa niaba ya wezake alimwomba mbunge awasaidie kutatua shida ya maji ambayo licha ya kupatikana mbali, wamekuwa wakiuziwa kwa bei kubwa.
Chanzo: HabariLeo