Waziri wa Afya nchini Malawi, Peter Kumpalume, amewasimamisha kazi zaidi ya maafisa 60 baada ya mamilioni ya dola kutoka Marekani, zilizotolewa kukabiliana na maradhi hatari ya Ukimwi na HIV, kupotea.
Bw Kumpalume, amesema kuwa ameanzisha uchunguzi baada ya kituo kinachofadhili mpango huo cha Marekani cha kukabiliana na kuzuia kuenea kwa maradhi hayo (CDCP) kuandika barua kulalamika.
Ameambia gazeti la Daily Times kwamba waliosimamishwa kazi ni maafisa wakuu katika idara za fedha na nguvu kazi katika wizara ya afya.
Wamesimamishwa kazi ili kutoa fursa kwa wakaguzi wa hesabu kufanya uchunguzi.
Balozi wa Marekani nchini Malawi, Virginia Palmer, amesema kupitia Facebook kwamba ana matumaini wezi wa fedha hizo watatambuliwa haraka iwezekanavyo, ili maafisa waaminifu wajulikane.
Malawi ni moja ya mataifa yenye viwango vya juu zaidi vya maambukizi ya Ukimwi duniani.
Hata hivyo, imekuwa ikipiga hatua na imepunguza kiwango cha maambukizi kutoka zaidi ya asilimia 12 mwaka 2004 hadi asilimia 10 mwaka 2014.
 
Top