Miaka ile ya 1980 nilikuwa nasoma sana magazeti ya kimataifa kama 'Africa' Africa Now', Africa Events' na mengineyo yaliyoruhusiwa kuingia nchini.
Haikuwepo mitandao ya kijamii kama ilivyo leo wala mawasiliano ya kompyuta,
hivyo tulipata habari nyingi za kimataifa kupitia magazeti ya kimataifa.
Ni katika magazeti hayo, nilisoma habari za mwanajeshi mwenye cheo cha Meja
Jenerali, Muhammadu Buhari aliyeingia madarakani nchini Nigeria kwa mapinduzi
Desemba 31, 1983. Miaka miwili ya utawala wake ilikuwa michungu kwa
wafanyakazi, madereva na wakorofi.
Siku chache baada ya kuweka mambo sawa yaani kuunda Baraza la Kijeshi,
‘mjeshi’ huyo alifanya ziara kwenye kampuni moja ya umma (nadhani ya mafuta),
ambapo yeye na msafara wake walifika mapema kabla ya baadhi ya wafanyakazi na
wakurugenzi.
Hakuwaacha hivi hivi, aliamuru wanajeshi kuwachapa viboko wote waliochelewa
kufika.
Buhari aliruhusu wanajeshi kwenda barabarani kufanya kazi ya Askari wa
Usalama Barabarani. Tofauti yao ni kwamba wao, hawakuwa wanasimama kuruhusu
magari kupita bali walikuwa wanawafuata madereva wanaokiuka sheria na
kuwacharaza bakora sawasawa. Halafu aliwatawanya askari kwenye ofisi za umma
ambako wafanyakazi waliojijengea utamaduni wa kuchelewa kazi walikula bakora.
Huyo ni Muhammadu Buhari wa wakati ule. Niliposikia ametangazwa mshindi wa
kiti cha urais, katika uchaguzi mkuu wa kidemokrasia Nigeria hivi karibuni,
haraka nilikumbuka bakora kwa madereva, kurushwa kichura kwa maofisa kama adhabu
kwa kuchelewa kwao na kuamuru kunyongwa wauzaji ‘unga’ na kulazimisha usafi kwa
kuwatia jela vikojozi wa barabarani.
Ingawa kuna watu walifurahia alivyosimamia nidhamu, wanajeshi wenzake
walimpindua mwaka 1985 na akazuiwa nyumbani kwake. Najiuliza, mjeshi huyu
hatapenda kuchota mambo ya zamani na kuyatumia sasa akiwa rais wa kuchaguliwa?
Wampenda, wamgeuka
Siku za mwanzo za utawala wake, wananchi walimfurahia Buhari aliyetarajiwa
kuondoa matatizo makubwa ya kiuchumi yaliyokithiri wakati wa utawala wa kiraia
wa Shehu Shagari, lakini hatua kali alizochukua kukomesha uzembe, kufukuza
wahamiaji, kucharaza viboko maofisa, alikasirisha wengi.
Ilionekana wananchi walihitaji mabadiliko makubwa ili kuondoa dhuluma,
ufisadi, uzembe, utovu wa nidhamu uliokithiri enzi za Shehu Shagari, lakini
alipoanzisha kampeni iliyoitwa “Vita Komesha Utovu wa Nidhamu” ambayo iliwagusa
wanasiasa na wafanyabiashara wengi, wakashitakiwa kwa rushwa kwa lengo la kuipa
heshima Nigeria, alichukiwa.
Utawala wake ulizuia uhuru wa habari, vyama vya siasa na vyama vya
wafanyakazi. Hivyo, alipopinduliwa Agosti 27, 1985 na ‘mjeshi’ mwingine Meja
Jenerali Ibrahim Babangida, wengi walipokea habari hizo kwa shangwe. Baada ya
kupinduliwa alizuiliwa nyumbani kwake katika mji wa Benin hadi mwaka 1988.
Buhari hakupotea kwenye siasa, alianza kufuata nyayo za mwanajeshi mwingine
Olusegun Obasanjo, ambaye baada ya kutawala kijeshi kuanzia Februari 13, 1976
hadi Oktoba 1, 1979 alirejea kutawala kama raia kuanzia Mei 29, 1999 hadi Mei
2007. Hali hiyo ilimvutia Buhari, akawania urais kama raia mwaka 2003 lakini
aliangushwa na Obasanjo wa chama cha People’s Democratic Party (PDP).
Matokeo yalimpa hamasa ya kugombea tena mwaka 2007 na aliangushwa na mgombea
wa PDP, Umaru Yar’Adua katika uchaguzi ambao mchakato wake ulishutumiwa na
waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kwamba ulitawaliwa na ukiukwaji wa
taratibu. Hakukata tamaa, alijitosa kwa mara ya tatu, mwaka 2011 pia
alipigwa mwereka na Goodluck Jonathan wa PDP.
Udhaifu alioonyesha Jonathan katika kupambana na rushwa na zaidi vita dhidi
ya kundi la kigaidi la Boko Haram, ulitumiwa na Buhari kama mtaji wa kisiasa.
Mwaka 2014 aliteuliwa na Chama cha All Progressives Congress (APC) kuwa mgombea
urais uliopangwa Machi 28, 2015. Vitu vilivyomwongezea mtaji na mvuto kwa
wapigakura ni heshima aliyojijengea kwamba si fisadi, kwamba kati ya madikteta
waliotawala Nigeria, yeye hakuwahi kufuja fedha za umma.
Aliwahi kuwa mkuu wa nchi akiwa na magwanda na kwa sasa wanaamini kuwa
ataweza kupambana na Boko Haram.
Japokuwa kulikuwa na wagombea wengine 14 wa urais, ushindani ulikuwa kati ya
Buhari na Jonathan wa PDP. Jonathan aliangushwa na Buhari kwa tofauti ya kura
milioni 2.5. Kwa anguko hilo, Jonathan amekuwa rais wa kwanza kushindwa katika
uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa amani.
Changamoto
Buhari amerithi mikoba ya Jonathan huku nchi ikiwa inakabiliwa na changamoto
kadhaa na kubwa zaidi ni usalama (kupambana na Boko Haram), kushuka bei ya
mafuta (asilimian 70 ya mapato ya Serikali yanatokana na mafuta), na kushuka
thamani ya naira (fedha za Nigeria).
Chanzo mwananchi