Filimbi ya kuanzisha mbio za uraisi kwa tiketi ya CCM itapulizwa Mei 23 baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu yachama hicho tawala huku makada sita walio' kifungoni 'wakitarajia kujua hatima yao kwenye mbio hizo 20
CCM imekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa uchaguzi, unaohusisha ratiba ya
chama hicho, kupitishwa kwa Ilani ya Uchaguzi na taratibu nyingine za kugombea
uongozi, kiasi cha kutia wasiwasi baadhi ya wanachama wake, wakiwamo makada
sita ambao walifungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kujihusisha na kuwania madaraka
baada ya kubainika kukiuka taratibu.
Makada hao waliopewa adhabu na Kamati Kuu ni mawaziri wakuu wa zamani,
Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine Steven waziri, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula, January
Kamamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia) na William Ngeleja, ambaye
alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Mbali na makada hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba aliwahi
kupewa barua ya katazo la kufanya ziara na mikutano ya kibinafsi yenye
viashiria vya kampeni za urais.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuthibitisha kuwapo
kwa vikao vya vyombo hivyo viwili wiki mbili zijazo.
“Kwanza habari hizo siyo za kweli, nazisikia kwa mara ya kwanza kutoka
kwako,” alisema Nape alipoulizwa kuhusu tarehe za vikao hivyo.
“Kwanza umeshaandika stori yenu halafu ndiyo mnanipigia kuthibitisha.
Inakuwaje msemaji wa chama hana habari, halafu nyinyi Mwananchi muwe nazo?”
alihoji Nape.
Hata hivyo, habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa
Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20, kuandaa taratibu zote za uchaguzi na siku
inayofuata, yaani Mei 21 iwasilishe kwenye kikao cha Halmashauri Kuu
kitakachokuwa cha siku mbili.
Habari hizo zinaeleza kuwa vikao hivyo viwili vinatarajiwa kutoa ratiba na
utaratibu wa kuchukua na kurudisha fomu kwa waombaji wa nafasi za udiwani,
ubunge na urais na kupokea na kupitisha ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya CCM kimelieleza gazeti hili kuwa vikao
hivyo vitahitimisha suala la wagombea sita wa urais waliopewa onyo kali kwa
kuanza kampeni mapema na kushiriki vitendo vya utovu wa nidhamu.
Habari kutoka ndani ya CCM pia zinaeleza kuwa katika eneo la mchakato ripoti
za Kamati Ndogo ya Maadili, chini ya makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula
itatikisa vikao hivyo hasa uchunguzi wake kuhusu mienendo na harakati za
kuwania urais
Wasiwasi na shauku ya ripoti ya kamati hiyo inatokana na kauli za hivi karibuni
za Mangula kuwa chama hicho kinazo taarifa za makundi ya makada wanaosaka urais
na matumizi makubwa ya fedha.
Makada hao, ambao miongoni mwao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa
kupeperusha bendera ya CCM kwenye mbio za urais, walidaiwa kukiuka taratibu
inayozuia wanachama kuanza kampeni mapema na adhabu yao ilitakiwa imalizike
Februari mwaka huu, lakini ikaongezwa kwa maelezo kuwa Kamati ya Maadili bado
inaendelea na uchunguzi.
Mbali na makada hao sita, wengine wanaotajwa kuwa na nia ya kuchukua fomu ni
aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emmanuel Nchimbi na
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha ambao jana walitangazwa
kusafishwa dhidi ya tuhuma za kutowajibika katika Operesheni Tokomeza. Wawili
hao walilazimika kuachia ngazi mapema mwaka jana baada ya Kamati ya Bunge kutoa
taarifa ya uchunguzi wake kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu
uliokuwamo kwenye operesheni hiyo iliyolenga kupambana na ujangili.
Vilevile, vikao hivyo vinatarajiwa kupokea na kujadili mapendekezo ya Ilani
ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha 2015-2020.
Vyanzo vingine vya habari vimeeleza kuwapo pia kwa ajenda ya hali ya siasa
inayohusishwa na misuguano ndani ya chama bara na visiwani, uandikishaji
wapigakura, mchakato wa Katiba mpya na jinsi ya kupambana na wapinzani, hasa
Ukawa.
Kamati Kuu inatarajia kutumia vikao hivyo kuangalia namna ya kupata wagombea
watakaokubalika kwa wananchi kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha urais, wabunge
na madiwani.
Chanzo Mwananchi