Kama ilivyozoeleka katika jamii zetu za Kiafrika, baba
ndiye nguzo ya familia ingawa katika huduma za afya zinamweka mama na mtoto
katika makundi maalumu katika kupata huduma za afya.
Wasomaji wa Piramidi ya afya, mwaka
mpya na mambo mapya. Baada ya kuongelea mambo mengi yanayomhusu mama na mtoto
kwa takriban miaka miwili, sasa tunamgeukia baba (mwanaume).
Kama ilivyozoeleka katika jamii zetu
za Kiafrika, baba ndiye nguzo ya familia ingawa katika huduma za afya zinamweka
mama na mtoto katika makundi maalumu katika kupata huduma za afya.
Kupitia kona hii nitawaletea
mfululizo wa makala zinazotoa ufahamu kuhusu matatizo mbalimbali ya kiafya kwa
wanaume.
Wanaume wanahitajika kuwa na
tahadhari kuhusiana na afya zao, kwani unapowalinganisha na wanawake na watoto,
wao wako katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali.
Jambo ambalo hata halihitaji utafiti
wa kisomi, jaribu kupita katika maeneo ya burudani utagundua robo tatu ya
wateja ni wanaume.
Wanaume ndiyo “wanaopiga maji” na
kuvuta sigara kwa wingi na ndiyo wanaokuwa na uchaguzi wa tabia hatarishi za
kupata matatizo ya kiafya.
Tabia hatarishi ni kama vile kuwa na
wapenzi wengi na upande mwingine ndiyo wanaowindwa zaidi na madada wanaofanya
ukahaba.
Kutokana na uwezo wao wa kufanya
kazi na kujiingizia kipato kikubwa, wanaume wana uwezo wa kufanya chochote kwa
kufanya ushawishi wa anasa mbalimbali.
Uwezo walio nao huweza kuwafanya
wale vyakula kiholela bila kuzingatia kanuni za afya, ulevi kupindukia, hivyo
kuwa na uzito mkubwa uliokithiri au kunenepa sana.
Maumbile ya kiume na mfumo mzima wa
homoni zake, unamfanya mwanaume kuwa na mrundikano zaidi wa mafuta ndani ya
mwili katika viungo kama moyo, ini na figo. Hii ni tofauti na mwanamke.
Hii ni moja ya sababu za wanaume
wengi kuwa na magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, kisukari, maradhi sugu ya
figo, kiharusi, magonjwa ya akili na unene ulipitiliza.
Wanaume pia huwa na maradhi ambayo
huwapata wao pekee. Magonjwa hayo ni kama vile saratani ya tezi dume na kiasi
kidogo cha homoni ya kiume iitwayo kitabibu ‘testosterone’.
Homoni hii ina umuhimu mkubwa kwa
mwanaume. Ndizo inayomfanya aonekane mwanaume mwenye misuli iliyoshiba na
kukomaa na uwezo wa kutengeneza na kuzalisha mbegu za kiume, ambazo ni muhimu
kufanikisha urutubishaji wa yai la mwanamke na kutunga mimba.
Magonjwa mengine ambayo yanawapata
zaidi wanaume kuliko wanawake ni kama vile saratani ya utumbo mpana na mapafu.
Maradhi haya yanaweza kuzulika kama uchunguzi au ugunduzi wa awali utafanyika.
Wanaume ndiyo wanaoathirika zaidi
kiakili pale viungo vya uzazi vinapoathirika. Moja ya jambo ambalo
mwanaume hatapenda kulisikia limpate ni kupungukiwa kwa nguvu za kiume na
kukosa uwezo wa kumpa mimba mwanamke.
Yapo maradhi ambayo yanayoweza
kuleta matatizo katika viungo vya uzazi na kusababisha mwanaume ashindwe
kusisimka kwa tendo la ndoa, kuishiwa nguvu za kiume, kukosa hamu ya tendo,
kutoa mbegu chache au zisizokomaa.
Maradhi hayo ni kama vile kisukari,
magonjwa ya mishipa ya damu, msongo wa mawazo, kuzaliwa na maumbile yasiyo
timilifu ya uzazi, ajali katika mfumo wa fahamu, maungo ya uzazi na matatizo ya
homoni.
Kutofanya mazoezi ndiyo chanzo cha
matatizo mengi ya kiafya, ikiwamo kisukari na maradhi ya moyo.
Chapwa: Mwananchi