Kada wa CCM aliyetangaza nia ya kugombea Urais kupitia chama hicho wiki iliyopita, Dr Muzzammili Kalola, juzi alionja joto ya jiwe baada ya kupata kipigo kutoka kwa vijana wa ulinzi wa Green Gurd wakati akisaka wadhamini mkoani Tanga.

Akisimulia mkasa huo kwa mwandishi wa NIPASHE kwa njia ya simu jana, alisema , Jumatano baada ya kuwasili nje za ofisi hizo kama alivyotakiwa na Katibu wa wilaya hiyo, ghafla alivamiwa na kundi la Green Guard wakimtaka aondoke.
 Dk Muzzammili Kalokola
Alisema walimshambulia kwa kumpiga kisha kumkata mtama na kudondoka, huku Katibu Mwenezi wa Wilaya, akitamka aondolewe katika eneo hilo kwa madai kuwa ‘Mkutano hauwezi kuandaliwa na mwingine halafu mtu mwingine azungumze’.

Tukio la shambulio hilo pia limeonyeshwa katika mitandao mbali mbali ya kijamii, ambapo mtangaza nia huyo alionekana akipigwa na kundi hilo na kuondolewa.

Alisema katibu huyo aliwaeleza vijana hao wamwondoe lakini akiwa eneo hilo la tukio alimpigia simu katibu wa wilaya aliyemtaka awali afike hapo saa 6:00 mchana kuomba udhamini.

“Wakati Katibu wilaya akija eneo la tukio, niliwasiliana pia na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga (RPC) ambaye awali nilipeleka malalamiko yangu kwake dhidi ya hujuma ninazofanyiwa,” alisema.

Alisema baada ya katibu wa wilaya kufika alimpa simu na kuzungumza na RPC na baadaye alilazimika kwenda polisi na kupewa RB/Tan/58000/2015.

 “Kada mwenzangu ndiye anayenichafua, maana nimefika hapa nikavamiwa ghafla halafu jioni saa 12:00 huyo kada alikuja kuomba ridhaa ya wadhamini,” alisema.

Akielezea hujuma alizofanyiwa, Dk. Kalokola alisema baada ya kuchukua fomu Dodoma alipewa barua za utambulisho kwa kila katibu wa mkoa ili wakasaini daftari la wageni na hatua nyingine zifuate.

Alisema mwanzoni mwa wiki hii alienda ofisi ya katibu wa wilaya Tanga, ambapo huko alimkuta kaimu wake ambaye alimweleza kuwa, ofisi inamtayarishia mtangaza nia Bernald Membe na Amina Salum Ali.

Alisema baada ya maelezo hayo, kesho yake alimwandikia barua Katibu Mkuu wa chama Dodoma kwa sababu barua alizopewa zinaeleza wazi kuwa, kila mtangaza nia atendewe haki.

Alisema siku hiyo wakati akijiandaa kwenda kwa RPC wa Tanga, ofisi ya wilaya iliwatuma watu wakamwite.

“Niliwajulisha kuwa nitaenda baadaye kwa sababu nilikuwa naenda polisi, baadaye nilipoenda katibu wa wilaya sikumkuta nilirudi kesho yake asubuhi nikaambiwa kesho yake niende kwa ajili ya kukutana na wadhamini,” alisema na kuongeza:
“Kwa kuwa Alhamisi nilitakiwa kwenda Dar es Salaam kwenye kesi ya katiba, nilimuomba ifanyike siku hiyo ya Jumatano, alikubali na kunitaka saa 6:00 mchana nirudi ofisi hapo,” alisema.

Alisema muda ulipofika alienda ndipo alipoambulia kipigo hicho.

Kutokana na shambulizi hilo, kada huyo ametupa lawama kwa baadhi ya makada wenzake ambao wanatengeneza njia za kuelekea Ikulu kwa njia za kiujanja ujanja.

Pia alisema baadhi ya makada ambao wapo mikoani kutafuta udhamini, wamekuwa wakiwahujumu wengine kutokana na kitendo chao cha kuchukua wadhamini zaidi ya kiwango kilichowekwa.

“Wadhamini wanatakiwa kila mkoa ni 450 lakini unakuta kada mmoja anachukua wadhamini 1000 sasa sisi wengine tupate nini, hii ni hujuma, CCM iliangalie hili,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,  Zuberi Mwambeji, alithibitisha kuzungumza na mtangaza nia huyo siku ya tukio lakini hana uhakika na shambulio.

Alisema siku ya tukio mgombea alimpigia simu na kumweleza kuwa, alipofika ofisi hapo ili azungumze na wadhamini, alizuiliwa na ofisi za chama hicho.

“Aliniambia alifika hapo ili apate udhamini lakini alizuiliwa , suala la kushambuliwa sina uhakika nalo, kwa sababu uongozi wa ofisi ya chama ulimueleza utaratibu wa kupata wadhamini.

Alisema uchunguzi wao unaonyesha kuwa mtangaza nia huyo alikuwa hana uwezo wa kuwasaka wadhamini na kuomba atumie jukwaa la mtangaza nia mwingin.
 
Top