Viongozi wa chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Mkoani Rukwa wameamua kuachia ngazi kwa kujiuzuru, ambapo mwenyekiti wa chama hicho na katibu wa mkoa huo pamoja na baraza zima la uongozi la mkoa wametangaza kuwa watabaki kuwa wanachama wa kawaida, kwa kile
walichokidai kutoridhishwa na maamuzi ya makao makuu katika uteuzi wa nafasi ya
ubunge wa viti maalumu kupitia chama hicho.
Akiongea na waandishi wa
habari mjini Sumbawanga mwenyekiti wa Chadema wa mkoa wa Rukwa Bw Zeno Nkoswe,
amesema licha ya kutoridhishwa na uteuzi wa Aida Kenani kuwa mbunge wa viti
maalumu kutoka mkoa huo wa rukwa, pamoja na makao makuu ya chama kupewa taarifa
mapema kuwa kiongozi huyo hivi sasa amekuwa msaliti, kwani mara tu baada ya kura
za maoni amekuwa anakipigia debe chama cha TLP, lakini pia kutotekelezwa kwa
ahadi ya kuwalipa mawakala zaidi ya 1,000 waliosimamia uchaguzi kwenye vituo
mbalimbali, pia imekuwa sababu ya wao kujiuzuru nafasi zao.
Kwa upande wake katibu wa
Chadema wa mkoa wa Rukwa Bw Ozem Chapita, akitoa ufafanuzi wa hatua hiyo
amesema uteuzi wa mtu ambaye anaonekana ni msaliti, kunaweza kukaathiri hata
uwezekano wa chama hicho kilichoshinda viti kumi kati ya tisa vya udiwani, kuweza
kuiendesha halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga kwa kuwa na meya wa manispaa,
kwa kushindwa kupata kura za kutosha.