Watu saba wamefariki dunia, wilayani kilwa, kufuatia boti waliyokuwa wakisafiria kutoka mji wa mkongwe wa Kivinje kwenda kisiwa cha Songosongo kuzama baharini.
Habari za uhakika kutoka
wilayani humo na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo na Kamanda
wa Polisi mkoani hapa, Renatha Mzinga (pichani), zinaeleza ajali hizo mbili
zinazofanana zimetokea juzi saa 2:30 asubuhi.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali
hiyo akiwemo mwenyekiti wa mji mdogo wa Kivinje, Mohamedi Peta na walioshiriki
kuokoa abiria hao, wameliambia gazeti hili kuwa, abiria hao wakiwamo wawili,
wenyeji wa Zanzibar, walikuwa wakitokea mji mkongwe wa Kivinje kwenda kisiwa
cha Songosongo katika shughuli za kibiashara.
‘Ajali hii iliyohusisha
wafanyabiashara wawili wa dagaa kutoka Zanzibar, walikuwa wakienda Songosongo
kununua bidhaa hiyo kwa ajili ya kupeleka nchi ya Kongo (DRC),’ alisema.
Mkuu wa wilaya hiyo, Njwayo,
akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, amekiri kutokea kwa vifo hivyo.
‘Taarifa hiyo ni ya kweli,
lakini nitashindwa kukuelezea kwa kina, kwani nipo nje ya wilaya yangu, hivyo
bado sijapata ripoti kamili kutoka kwa wataalamu wangu,’ alisema.
Alitaja chanzo cha ajali hiyo
ni kuchafuka kwa bahari, kunakochangiwa na upepo mkali unaoendelea kuvuma
kwenye Bahari ya Hindi.
Kamanda wa Polisi mkoani
Lindi, Mzinga alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokana na boti mbili
tafauti, ikiwemo mali ya Halmashauri ya wilaya ya Kilwa, inayotumika kutoa
huduma ya kusafirisha watu kati ya Kivinje na kisiwa hicho, iliyokuwa imebeba
abiria 16 wakielekea kisiwa cha Songosongo.
Aliwataja waliopoteza maisha
kuwa ni, Hassan Ally Fundi (40), mkazi wa Msinjahili, Manispaa ya Lindi na
Rashidi Zawena (36), mwenyeji wa mkoa wa Tanga.
‘Wavuvi hawa walikuwa
wanatumia boti ndogo inalofahamika kwa jina la Dingi, walikuwa wakirejea
baharini kuvua, walipofika karibu na maeneo ya pwani, walibadilisha chombo na
kutumia mtumbwi mdogo ili uwafikishe ufukweni, lakini kabla ya lengo lao
halijatimia mtumbwi ulipinduka na kupoteza maisha,’ alisema.
Aliwataja watu wengine watano
waliofariki na wakiwa kwenye boti ya halmashauri kuwa ni Asha Mahula, Eva
Ngwavi wengine watatu waliotambulika kwa jina moja moja, Mariamu, Zuwena na
Bishara.
CHANZO: NIPASHE