Dar es Salaam. Wakati operesheni ya kuweka alama ya X kwenye nyumba zilizojengwa mabondeni, maeneo ya wazi na kinyume na taratibu ikiendelea, Hoteli za Double Tree na Slip Way nazo zimekumbwa na pigo hilo.
Hoteli hizo pamoja na nyumba ya Maheshbhai Patel na baadhi ya wamiliki wengine wa nyumba ambao kuta zake zimejengwa karibu na barabara ya Slip Way eneo la Msasani Peninsula, wamepewa siku saba kuzibomoa.
Jana, uongozi wa Manispaa ya Kinondoni uliweka alama za X na kuwaonya wamiliki hao kwamba, wasipobomoa manispaa itazibomoa na kudai gharama za ubomoaji.
Mwandishi wetu alifika katika barabara hiyo na kukuta hoteli hizo na majengo mengine yakiwamo makazi ya watu, yamewekewa alama hizo katika sehemu ambazo zinatakiwa kubomolewa.
Tofauti na ilivyokuwa katika maeneo ya Jangwani juzi ya watu kufanya fujo hadi askari Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kulazimika kutumia mabomu kuwatawanya, mitaa ya huko ilikuwa tulivu.
Watu waliokutwa kwenye nyumba zilizowekwa alama ya X, hawakuwa tayari kuzungumzia wakisema siyo wahusika wakuu wa nyumba hizo.
Patel kwa upande wake, alisema kupitia mlinzi wake kwamba atafutwe Jumatatu, kuzungumzia notisi hiyo.
Akizungumza kwa simu jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema Serikali haitaurudi nyuma katika kutekeleza sheria hata kama kuna watu wana jeuri ya pesa.
Alisema Manispaa ya Kinondoni iliwapatia vibali vya kupendezesha maeneo ya pembezoni mwa barabara ikiwamo kupanda maua, lakini wao badala ya kutimiza masharti ya vibali walizungushia kuta jambo ambalo hawatalivumilia.
“Wangependezesha na kufunga minyonyoro kuzuia kuharibiwa mazingira yao kama walihisi wananchi wangeharibu, lakini siyo kujenga kuta.
“Nimewaagiza Kinondoni wawapatie notisi ya siku saba kubomoa kwa hiari. Wasisubiri Serikali ivunje.
Tutabomoa hadi lile jengo lililopo karibu na Hospitali ya Ami lililovunja sheria, yule hawezi kuonyesha jeuri ya fedha,” alisema Lukuvi.
Alisema Serikali ina mpango maalumu wa kubomoa majengo yote yaliyojengwa kinyume na sheria Masaki na Oysterbay na wameanza na Barabara ya Slip Way.
Katika hatua nyingine, sakata la bomoabomoa pia limewakumba waliojenga katika hifadhi za mikoko baada ya watumishi wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na maofisa misitu wa Manispaa ya Kinondoni kuweka alama ‘X’ katika nyumba zaidi ya 30 ikiwamo ya kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God, Dk Getrude Rwakatare.
Kazi hiyo ilianza jana mchana katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ikiwamo, katika Mtaa wa Ally Sykes, Kawe na Jangwani Beach eneo la Mbezi Beach. Ofisa Misitu Msaidizi wa Manispaa ya Kinondoni, Issa Juma aliwaambia wanahabari kuwa kazi hiyo ni endelevu.