ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chadema, Leticia Nyerere amefariki dunia.
Leticia alifariki dunia katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo Lanham, Maryland jana saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Taarifa za awali kutoka Marekani, ambako msiba huo umetokea, ziliarifu kuwa msiba upo DMV 9004 Brightlea Court, Lanham, MD 20706.
Msemaji wa familia hiyo, Mbunge wa zamani wa Chadema, John Shibuda alithibitisha kutokea kwa msiba huo. Alisema ndugu wanajipanga kukutana na kuamua cha kufanya.
“Ndugu yangu ni kweli msiba umetokea wa mpendwa wetu Leticia Nyerere, umetokea jana mchana huko Marekani na huku kwetu ilikuwa ni usiku, hivyo ndugu bado hatujakutana na kuamua kwa pamoja ni wapi tuweke msiba na lini tutazika,” alisema Shibuda.
Shibuda alisema kuwa leo familia itatoa taarifa kamili ya taratibu zote za msiba huo baada ya wanafamilia kukutana.
Magufuli ampa pole Mama Maria Wakati huohuo, Rais John Magufuli jana alimtembelea na kumpa pole mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere kufuatia kifo cha mkwewe, Leticia Nyerere.
Pamoja na kutoa mkono wa pole kwa Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli pia amewapa pole wanafamilia wote na amewaomba kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na ndugu yao.
Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alimueleza Rais Magufuli kuwa familia inaendelea na taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Marekani na itatoa taarifa baadaye.
Mwezi Julai mwaka jana, Leticia Nyerere alijiondoa rasmi Chadema na kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Leticia aliolewa na Madaraka Nyerere na kujaliwa kupata watoto watatu. Madaraka ni mmoja wa watoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Hata hivyo Leticia alitengana na Madaraka katika miaka ya mwisho ya 1990.
Chanzo: HabariLeo