Baada ya kuanza kwa kasi zoezi la ‘utumbuaji majipu’ katika sekta ya fedha, mkazo ukiwa zaidi katika kuzuia ukwepaji kodi katika Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA) zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Rais John Magufuli anajiandaa kushughulikia tatizo la ufisadi katika ngazi ya Halmashauri za Manispaa na Miji.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Magufuli jijini juzi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani) alisema bado kuna “majipu mengi serikalini” ikiwemo kwenye halmashauri mbalimbali na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya tano itahakikisha inayatumbua yote. Lukuvi aliyasema hayo wakati wa mkesha wa mwaka mpya ulioandaliwa na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali, kwenye Uwanja wa Uhuru.
Mkesha huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini kutoka ndani na nje ya nchi, na mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Rais ambaye aliwakilishwa na Lukuvi. Majipu ambayo Rais Magufuli anataka kuyatumbua yako kila mahali, alisema Lukuvi na kueleza imekuwa kawaida kuona dawa zinaibiwa katika hospitali na zahanati.
Aidha, Lukuvi alisema watumishi wa serikali hawawajibiki ipasavyo hasa kwenye halmashauri, ambako huiba fedha za umma na kutoa huduma kwa misingi ya rushwa. “Haya majipu yote tunaishi nayo na wote tunayajua, wakati Rais akitumbua majipu makubwa sisi tumsaidie kuvitumbua vijipu vidogo vidogo ambavyo tunaishi navyo lengo ni kuhakikisha rasilimali za nchini zinawanufaisha wananchi wote,” alisema.
Lukuvi aliwaasa viongozi wa dini waendelee kuielimisha jamii kuishi maisha yenye maadili na kuachana na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma na matumizi ya dawa za kulevya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkesha huo, Mchungaji Godfrey Malassu alisema ni mwaka wa 18 sasa tangu kuanzishwa kwa mikesha kama hiyo ya kuliombea taifa ambayo hujumuisha Watanzania bila kujali madhehebu yao.
Aidha, alisema sadaka iliyopatikana kwenye mkesha huo itaelekezwa kusaidia upatikanaji wa nishati ya umeme wa jua hospitali mbalimbali za Tabora Mjini.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye aliwataka Watanzania kukinunua kitabu kilichoandaliwa na kanisa hilo cha ‘Ijue siri ya amani ya Taifa’ kilichokuwa kinauzwa uwanjani hapo ili kiwasaidie kutambua umuhimu wa amani.
Mbali na kudhibiti ulipaji kodi katika Bandari ya Dar es Salaam, Rais pia amechukua hatua kadhaa za kuminya ubadhirifu katika ngazi ya Serikali kuu, ikiwa ni pamoja na kutoa mwezi mmoja tangu Novemba mwaka jana, watumishi wa umma wawe wamejaza fomu za tamko la mali na madeni yao na ambaye hatafanya hivyo angechukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu.
Mbali na agizo hilo, watumishi wa umma wamekuwa wakibanwa na hatua za Rais Magufuli za ubanaji matumizi ya serikali ambapo masuala kama ya safari zisizo za lazima na vikao vya kuhalalisha posho vimefutwa.
Baraza la Maadili linatarajiwa kuwaita viongozi na watumishi wa umma watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao wa kujaza fomu hizo ili wajieleze na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwamo kuwabaini wale wote walioainisha taarifa za uongo.
Chanzo: Nipashe