Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza ametangaza vita dhidi ya biashara za magendo na kueleza ameshapokea majina ya watu 16 ambao atalala nao mbele mwaka huu wa 2016.
Mbali na vita dhidi ya biashara ya magendo, Mahiza pia ameahidi kupambana na wauzaji wa dawa za kulevywa.
Alisema amepokea majina hayo ya wafanyabiashara nguli wa magendo na sasa ofisi yake inaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi. Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo alisema serikali mkoani hapa imejipanga kudhibiti kikamilifu bandari bubu 19 zinazotumika kukwepa ushuru na uingizaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mahiza aliyaeleza hayo kwa waandishi wa habari juzi wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mpango mkakati wa maendeleo wa mkoa wa mwaka 2016/17, pamoja na kuwatakia heri ya mwaka mpya wananchi wa Tanga.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema biashara ya madawa ya kulevya imefika katika kiwango kibaya na uchunguzi umeonyesha kuwa jumla ya wakazi 867 wameathirika kwa matumizi ya dawa hizo.
Alitoa wito kwa kila anayejihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja kwa kuwa serikali imejipanga kupambana nao na hawatofanikiwa.
Alisema biashara hiyo imeshamiri kiasi kutishia uwapo wa nguvu kazi mkoani Tanga, na kudai serikali imeshajiwekea lengo la kutokomeza uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa mihadarati kwa kipindi cha mwaka 2016.
Ili kumudu hayo, serikali ya mkoa imejiwekea mipango mkakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu, alisema.
“Japo penye mafanikio hapakosi changamoto lakini tunamaliza mwaka 2015 tukiwa tumefanikiwa katika sekta za afya, elimu, maji, miundombinu na
uchumi kwa ujumla,” alisema Mahiza.
Wakati huohuo, mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza alisema serikali itahakikisha inawahamasisha wanannchi kujiunga na mifuko ya huduma za afya ili kuepukana na adha ya kupata matibabu kwa kulipa fedha taslimu.
Aidha, Mahiza alisema jumla ya Sh. bilioni 38 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maji mkoani Tanga mwaka huu na kwamba imeundwa kamati ya kufuatilia mienendo ya miradi hiyo ambayo italenga kutega maji katika mito, kuchimba visima na kuvuna maji ya mvua.
Chanzo: Nipashe