POLISI wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa inamshikilia mkazi wa kijiji
cha Ulinji, Manispaa ya Sumbawanga mwenye umri wa miaka 28 akituhumiwa
kumpatia ujauzito dada yake mwenye umri wa miaka 14 anayesoma darasa la
saba.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa ambaye amemtaliki mkewe, alirejea kuishi
nyumbani kwa wazazi wake kijijini Ulinji miaka miwili iliyopita kabla ya
kumpatia ujauzito mtoto huyo wa baba yake mkubwa.
Polisi imethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo juzi saa 8:20
mchana na kufikishwa katika kituo hicho cha Polisi. Alikamatwa na Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Ulinji, Manispaa ya Sumbawanga, Linus Mbutu.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ulinji, Mbutu alisema mtuhumiwa
alikamatwa na askari wa Mgambo wa kijiji hicho akiwa amejificha kwa saa
tatu porini akikwepa kukamatwa.
“Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na taarifa kutoka kwa walimu
ambako msichana huyo alikuwa akisoma baada ya kubainika kuwa ni
mjamzito,” alisema Mbutu.
Inadaiwa kuwa wazazi wa msichana huyo wakiongozana na Mwalimu Mkuu wa
shule anayosoma pamoja na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, walitoa
taarifa kituo cha Polisi mjini hapa na kupewa hati ya ukamataji yenye
namba 297, ambapo walipatiwa fomu ya matibabu (PF.3) kisha msichana huyo
akifanyiwa uchunguzi katika Zahanati ya Ulinji .
“Baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu mwanafunzi huyo alibainika
kuwa na ujauzito wa miezi minne …alipohojiwa alimtaja mshitakiwa ambaye
ni kaka yake akisisitiza kuwa walikuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa
muda mrefu,” alisema Mbutu.
Baba wa watoto hao (jina limehifadhiwa) alikiri kwamba kijana wake
huyo alikuwa ameoa lakini aliachana na mkewe na kurudi nyumbani, ambapo
aliendelea kuishi katika familia hiyo bila wao kujua kama watoto wao
wana mahusiano ya kimapenzi.
Alisema watoto hao walikuwa wakienda shambani kulima bustani ambako
inadaiwa ndiko walikuwa wakikutana na kufanya mapenzi kabla ya walimu
kugundua ujauzito wa binti huyo.
Baba huyo alisema mkasa huo umetia aibu kubwa familia yake na
wameachia Polisi ichukue hatua kutokana na kushindwa kuvumilia kitendo
cha kijana wao ambaye inadaiwa miaka miwili iliyopita, pia alimpa
ujauzito dada yake ambaye ni mtoto wa baba yake mkubwa.
Kwa upande wake mama wa watoto hao, alisema huo ni mkosi katika
familia yao na hawatawasamehe watoto hao kwa aibu waliyosababishia
familia.
Chanzo: HabariLeo