RAIS John Magufuli ‘ametumbua majipu’ katika Idara ya Uhamiaji nchini
baada ya kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester
Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na Fedha,
Piniel Mgonja ili kupisha uchunguzi katika idara hiyo nyeti nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ikimkariri Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni
Sefue jana jioni, Rais Magufuli amewasimamisha watendaji hao ili
kupisha uchunguzi kutokana na dosari alizozibaini Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga alipotembelea Idara ya Uhamiaji hivi
karibuni.
Balozi Sefue alitaja dosari hizo kuwa ni pamoja na tuhuma za rushwa,
ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji wa taratibu za
manunuzi na utendaji mbovu. Alisema watendaji hao wakuu wa Uhamiaji
wamesimamishwa mara moja hadi uchunguzi utakapokamilika na kwamba endapo
watabainika kutokuwa na makosa, Rais ataamua hatma yao.
Ambokile aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji Agosti 29, 2013.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemrejesha Eliakim Maswi kuwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, baada ya kukamilisha kazi maalumu
aliyomtuma kuifanya katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kabla ya kurejeshwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Manyara,
Maswi aliteuliwa kuwa Kaimu Naibu Kamishna Mkuu wa TRA. Katibu Mkuu
Kiongozi Sefue alisema Rais Magufuli amefanya mabadiliko hayo kwa lengo
la kumtafuta mtu mwenye utaalamu wa kuendeleza kazi aliyoifanya Maswi,
ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana, Rais Magufuli
alitangaza vita dhidi ya watendaji wa serikali ambao hawatekelezi
majukumu yao ipasavyo akitumia falsafa yake ya ‘kutumbua majipu’ na
kuwaomba Watanzania wamuunge mkono na pia wamwombee kwani siyo kazi
nyepesi.
Tayari amegusa idara na taasisi nyeti nchini kama vile TRA, Mamlaka
ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Shirika Hodhi la Usimamizi wa Reli (RAHCO), Shirika la Reli
Tanzania (TRL), ambako vigogo wake kadhaa wamepoteza kazi na wengine
kusimamishwa
Chanzo: HabariLeo