Edwin semzaba Enzi za uhai wake
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza
Mukandala ametoa salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Mhadhiri
chuoni hapo, Mwandishi na Muigizaji, Edwin Semzaba.
Profesa Mukandala alitoa salamu hizo jana chuoni hapo, mara baada ya
kumalizika kwa mkutano na waandishi wa habari uliohusu kongamano la saba
la wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Mukandala alisema, wanafamilia wa chuo hicho wana masikitiko
makubwa kutokana na kifo cha mwenzao Semzaba, ambaye pia alisoma naye
miaka mitatu shahada ya awali.
“Alikuwa Mwalimu mzuri na kipenzi cha wanafunzi. Ameandika maandiko mengi pia alikuwa ni muigizaji mzuri,” alisema.
Pia, alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa watumishi wa Idara yake ya
Sanaa na Sanaa za Maonesho chuoni hapo kwa kuwa alikuwa mfano mzuri wa
kuigwa kwa jinsi alivyoipenda kazi yake na kubobea.
Alisema, Watanzania walifurahia kazi yake na kusoma vitabu vyake alivyovitunga.
Ibada ya kumwombea marehemu ilifanyika katika Kanisa la Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam jana na baadaye kwenda kuzikwa katika makaburi ya
Kinondoni.