Agizo la Rais Dk. John Magufuli kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto la kutaka jengo lililokuwa likitumika kama ofisi ya kitengo cha afya ya uzazi na mtoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), lifanywe wodi ya wazazi ndani ya siku mbili, limewatoa jasho vigogo.
 
Vigogo kutoka wizarani na wakurugenzi wa Muhimbili, jana walikuwa wakihaha kutekeleza agizo hilo.
 
Tofauti na ambavyo ingetarajiwa kuwa uhamishaji samani na kupanga vitanda ungefanywa na watumishi wa ngazi za chini pekee, Nipashe ilishuhudia Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mpoki Ulisubisya, akihamisha samani zilizokuwa kwenye ofisi hizo ili iweze kutumika kama wodi ndani ya saa 48, alizotoa Rais Magufuli. 
 
Mbali na Ulisubisya, wakurugenzi wengine wa wizara hiyo na wale waliokuwa wakitumia jengo hilo, kila mmoja alionekana akifanya kazi kuhakikisha vifaa vilivyokuwa kwenye ofisi hizo vinahamishwa na vitanda vinawekwa.
 
“Hapa kazi tu si unaona tunatekeleza agizo la Rais? Tumekuja tangu asubuhi kutoa vitu vyote. Hapa hakuna mfanyakazi wa cheo chochote wote tunafanya kazi,” alisema mmoja wa wakurugenzi ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa madai si msemaji.
 
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, akizungumza jana baada ya kutembelea jengo hilo na kuona uondoaji samani unavyofanyika, alisema baada ya kutekelezwa kwa agizo la Rais, hakuna mgonjwa atakayelala chini.
 
“Tumeanza asubuhi na matarajio yetu itakapofika jioni (jana) tutamaliza na kukabidhi kwa uongozi wa Muhimbili kwa ajili ya kuboresha  kabla ya kuweka vitanda,” alisema.
 
Akizungumza na waandishi wa habari wakati akiendelea kutoa samani hizo, Katibu Mkuu Ulisubisya alisema kazi ya kuhamisha samani kwenye jengo hilo, ilianza jana asubuhi na walitarajia kuimaliza jioni. 
 
Alisema jengo hilo lenye ghorofa nne litakuwa na uwezo wa kuwa na vitanda kati ya 300 na 350 na kumaliza shida ya wagonjwa 40 waliokuwa wanalala chini kila siku.
 
“Juzi pekee kulikuwa na kinamama 180 lakini vitanda vilivyopo ni 120. Wengi walikuwa wanalala chini. Baada ya kutoa samani zote tutakabidhi jengo kwa uongozi wa Muhimbili kwa ajili ya matengenezo ikiwamo kuongeza bafu na sehemu za kufulia kwa kuwa awali ilikuwa ofisi ikiwa na vyoo pekee,” alifafanua.
 
Alisema eneo la kliniki ya afya ya uzazi na mtoto lililokuwa linatumiwa na madaktari  kuangalia afya za wajawazito, litatumika kwa mama wanaokwenda kunyonyesha watoto njiti na kwa jana tayari walikuwa wameweka vitanda 35.
 
Mmoja wa viongozi waliokutwa katika wodi hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa madai kuwa si msemaji, alisema kwa kuwa eneo hilo lilikuwa na choo, bafu na sehemu za kufulia litaanza kutumika kuanzia leo.
 
“Hadi sasa kama unavyoona tumeshaweka vitanda vitakavyotumiwa na mama wenye watoto waliolazwa ghorofa ya pili itakuwa rahisi kwenda kunyonyesha. Kule walikokuwa kulikuwa na vitanda 32 lakini wagonjwa wanafika 50 hadi 60 kwa siku,” alifafanua.
 
Alipoulizwa kuhusu mahali watakakohamishiwa watumishi waliokuwa wakitumia jengo hilo, Katibu Mkuu alisema baadhi watapelekwa wizarani na wengine kwenye ofisi za umma.
Chanzo: Nipashe
 
 
Top