Wanafunzi 930 na walimu 16 wa Shule ya Msingi  Ipinda wilayani Kyela, wanajisaidia vichakani baada ya shule hiyo kukosa huduma ya vyoo na maji safi kwa muda wa miaka saba.
 
Hatua hiyo imesababisha uongozi wa kata ya Ipinda  kutaka kuifunga kwa muda usiojulikana.
 
Walimu na wanafunzi hupata adha pindi wapatapo shida ya  kujisaidia kwa kuwa  wengi hutembea umbali mrefu kwenda kwenye nyumba za jirani na shule kufuata huduma ya vyoo huku wengine wakilazimika kwenda vichakani karibu na shule hiyo ili kujisitili.
 
Walimu wa shule hiyo, Suma Kasyuka na Ally Mwaisusa, walisema kwa zaidi ya miaka mitano wamekosa huduma ya vyoo na maji safi kutokana na vyoo vilivyokuwepo kujaa. Walisema hatua hiyo imesababisha kukosa msukumo wa kufundisha, hivyo kuiomba  serikali kupitia halmashauri ya wilaya kutatua tatizo hilo. 
 
Nao Lweyemam Lwuchus na Eliud Mwalukuta, walisema shule hiyo licha ya kukosa vyoo na maji safi, imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa na vitabu.
 
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Raha Brown, alisema toka ahamishiwe hapo na kupewa cheo hicho miaka mitano iliyopita, shule ilikuwa na tundu moja tu la choo cha walimu ambalo ni bovu huku choo cha wanafunzi kikiwa kimejaa. Alisema wamefanya  vikao kadhaa kujadili hali hiyo lakini hakuna matokeo yoyote.
 
Alisema ni heri shule hiyo ifungwe ili kupisha ujenzi wa vyoo kuwanusuru wanafunzi 930 na walimu 16 dhidi ya magonjwa ya milipuko. Kutokana na hali hiyo, alisema eneo zima la shule limetapakaa vinyesi huku harufu ikiwa mbaya hivyo kuwakosesha raha ya kufanya kazi kwa ufasaha.
 
Halima Sanga, Rebeca Castrol, Bruno Jackson na Edgar Castor ambao ni  wanafunzi wa darasa la saba,  kwa nyakati tofauti walisema hawana raha ya kusoma kutokana na matatizo yaliyopo, likiwamo  la ukosefu wa vyoo. 
 
Walisema ni bora shule hiyo ifungwe ili viongozi wa kijiji wakae na wazazi kwa kuwashirikisha viongozi wa ngazi ya wilaya kutafuta suluhisho la tatizo hilo.
 
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ipinda, Cuthbert Mwalukama, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na wameshafanya vikao kadhaa ambavyo vimeamua vyoo vijengwe haraka. 

 
Top