WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amemwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Bohari Kuu ya Dawa
(MSD), kuwasimamisha kazi mara moja wakurugenzi wanne wa taasisi hiyo
kutokana na tuhuma za kuwepo matumizi mabaya ya Sh bilioni 1.5.
Wakurugenzi hao ni Mkurugenzi wa Kanda wa MSD, Cosmas Mwaifwani,
Mkurugenzi wa Fedha, Joseph Tesha, Mkurugenzi wa Ugavi, Misanga Muja na
Mkurugenzi wa Manunuzi, Heri Mchunga.
“Naomba uwaandikie barua za kuwasimamisha wakurugenzi hawa wanne ili
wapishe uchunguzi wa matumizi mabaya ya Sh bilioni 1.5 za MSD,” alisema
Ummy alipozungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam.
Ummy alisema taarifa alizonazo ni kwamba kiasi hicho cha fedha,
kilitumika kununulia dawa kinyume cha utaratibu na Sheria ya Manunuzi ya
Umma, hivyo kuna haja ya kufanyika kwa uchunguzi huo.
Uamuzi wa Waziri huyo wa Afya ni mwendelezo wa hatua kadhaa
zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano dhidi ya watumishi wa umma
ambao wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu kwa
kuchukuliwa hatua katika kile ambacho Rais John Magufuli amekipachika
jina la ‘kutumbua majipu.’
Utekelezaji agizo la Magufuli Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ya
kuwapatia vitanda wanaokwenda kujifungulia katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili jijini Dar es Salaam, jana ilitekelezwa baada ya MSD kupeleka
vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 89.
Vifaa ambavyo alivikabidhi jana Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean
Bwanakunu ni vitanda 120, magondoro 120, vitanda 10 vya kujifungulia,
mashuka 840 na vitanda kwa ajili ya watoto njiti 10.
“Tumeleta vifaa hivi hapa baada ya kuagizwa na Rais kuwa tulete vifaa
hivi kwa ajili ya wodi ya wanawake na Rais ametuhakikishia kuwa fedha
hiyo italipwa mara moja,” alisema Bwanakunu wakati akikabidhi vifaa
hivyo ambavyo vilipokewa na Waziri Ummy.
Rais alitoa ahadi ya kuwapelekea vitanda wanawake hao baada ya kupita
katika wodi hiyo, wakati anatoka kumjulia hali Mufti wa Tanzania, Shehe
Abubakary Zubeiry.
Akihutubia Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki,
Rais Magufuli aliahidi kuwa ahadi yake ya kuwapelekea vitanda wajawazito
hao ataitekeleza haraka.
Akipokea vifaa hivyo, Waziri Ummy alimshukuru Rais kwa kuguswa na
afya ya wanawake baada ya kupita katika wodi ya wazazi na kukuta baadhi
yao wakilala chini.
Alisema akiwa waziri aliyepewa dhamana ya kuongoza wizara hiyo,
amefurahishwa kuona Rais hataki masuala ya urasimu ya mchakato, bali
anataka kuona mambo yanatekelezwa kwa vitendo.
“Baada ya kupokea vifaa hivi, nakuagiza Mkurugenzi wa Muhimbili,
kwamba vitanda hivi vifungwe leo, na akina mama ambao wamebanana kule
wodi ya wazazi wahamishiwe katika jengo lingine ambalo litakuwa na
vitanda hivi,” alisema Ummy.
Alisema kwa vitendo alivyoonesha Rais Magufuli, atahakikisha kuwa
huduma za afya zinatolewa kwa kiwango ambacho wananchi wanapenda
kitolewe.
“Rais ameguswa na matatizo ya wananchi wake, sisi ambao tunamsaidia
lazima tuwajibike na amenipa msukumo wa ajabu kushughulikia changamoto
zinazozikabili hospitali zetu,” alisema.
Hospitali za mikoa na wilaya kukaguliwa Waziri Ummy alimwagiza Katibu
Mkuu wa Wizara yake, Dk Mpoki Ulisubisya kumwagiza Mkurugenzi wa Tiba
wa wizara hiyo, ahakikishe anakwenda mikoani kukagua matatizo ya
hospitali za mikoa na wilaya na kutoa suluhisho la changamoto hizo.
“Badala ya kwenda nje ya nchi, katibu mkuu mwagize mkurugenzi aende
wilayani na mikoani huko akajionee hali halisi za hospitali zetu ili
tuweze kushughulikia changamoto hizo,” alisema Ummy.
Pia alimwagiza katibu mkuu kwa kushirikiana na mkurugenzi huyo wa
Tiba kutoa taarifa kila siku za hali za hospitali za mikoa na wilaya
kama kuna wagonjwa ambao wanalala chini ili watatuliwe matatizo.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kutoa taarifa wizarani kila siku
kama katika maeneo yao kuna mgonjwa anayelala chini katika hospitali za
wilaya na mikoa. “Sitegemei tena mgonjwa alale chini,” alisema
Chanzo: HabariLeo