WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
amewasimamisha kazi watumishi wawili wa Shirika la Utangazaji la Taifa
(TBC) kutokana na utendaji usioridhisha.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TBC Dar es Salaam
jana, Nape aliwataja watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni Mkurugenzi
wa Idara ya Habari na Matukio, Mbwilo Kitujime na Meneja wa Vipindi,
Edna Rajab ambao wamesimamishwa kazi na uamuzi huo utafikishwa kwa Bodi
ya TBC kwa hatua zaidi.
“Tunachukua uamuzi wa kuwasimamisha kazi watendaji hawa ili kujenga
upya Idara hii muhimu katika ustawi wa TBC na habari kwa ujumla,”
alisema Nape.
Aidha, Waziri huyo amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TBC kuwachukulia
hatua watumishi wengine walio chini ya Idara hiyo kwa kuwa wako chini ya
mamlaka yake na kutoa mrejesho wa hatua alizochukua dhidi ya wale wote
wilioonesha utendaji mbovu.
Alisema Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na kuwepo kwa
malalamiko ya muda mrefu juu ya utendaji mbovu na wa kutoridhisha
viongozi na baadhi ya watumishi wa Idara hiyo hivyo hatua hizo
zimechukuliwa ikiwa ni kujenga upya na kuboresha Idara hiyo muhimu
katika uendeshaji wa shirika lolote lile la Habari na kuongeza ufanisi.
Idara ya Habari na Matukio ya TBC inaundwa na Mkurugenzi wa Idara, Meneja wa Vipindi, wahariri na waandishi wa habari.