Serikali inatarajia kutoa ajira 40,000 kwa walimu wa shule za msingi na sekondari mwaka huu.
 
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo, alilieleza Nipashe jana kuwa idadi hiyo inalenga kupunguza upungufu wa walimu shuleni.
 
Jaffo alisema ajira hizo zitatangazwa mapema mwaka huu na zitaongeza nguvu kwenye shule zenye uhitaji wa walimu hasa mpya na zile zilizoandikisha wanafunzi wengi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza.
 
Sambamba na hilo, ameahidi kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuwezesha wanafunzi zaidi ya 5,800 wa Shule ya Msingi Majimatitu wanapata elimu bora.
 
Alisema idadi hiyo ya wananfunzi ni sawa na idadi ya shule sita za msingi, hivyo itagawanywa katika shule za jirani pamoja na kujenga madarasa mapya katika shule hiyo.
 
“Ongezeko hili la wanafunzi waliojiandikisha darasa la kwanza mwaka huu limetokana na mfumo wa serikali kutoa elimu bure na lengo la serikali ni kutoa elimu bora, hivyo kama serikali tutahakikisha tunaboresha mazingira kwa kuweka madawati ya kutosha, madarasa na walimu, hivyo hakuna mwanafunzi atakayekaa chini kuanzia mwezi wa sita,” alisema Jaffo.
 
Pia alisema serikali itahakikisha inaongeza majengo katika shule hiyo pamoja na kujenga shule mpya umbali wa kilomita moja kutoka shule hiyo ilipo, katika kiwanja kilichotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Martin Lumbanga, kwa ajili ya kujenga shule mpya.
 
Alimtaka Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Photidas Kagimbo, kuangalia uwezekano wa kujenga jengo la ghorofa katika kiwanja hicho ili kukidhi mfumuko wa wanafunzi wanaoandikishwa kila mwaka pamoja na kupunguzia wanafunzi wa Shule ya Mbagala Majimatitu katika shule hiyo mpya.
 
Pia aliwataka kuwashirikisha wamiliki wa viwanda wa manispaa hiyo, mchakato wa ujenzi wa madarasa ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
 
Jafo pia alimtaka Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Angel Frank, kuhakikisha walimu wa shule hiyo wanaotakiwa kupandishwa daraja wanafanyiwa hivyo pamoja na kulipwa mishahara stahiki kwa wakati kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kulea watoto hao. 
 
Naye Mkuu wa shule hiyo, Abdallah Ngomi, alisema shule  ina zaidi ya wanafunzi 5,800, walimu 77 wakati mahitaji yakiwa ni walimu 131 na madawati 900 hali inayowalazimu kuweka madawati 52 katika darasa moja badala ya 15 huku mahitaji ya  kwa shule nzima yakiwa ni 1,959.
 
“Tuna uhitaji wa vyumba vya madarasa 131 na kwa sasa tunavyo 22 pekee na tunatarajia kujenga 10, hivyo mahitaji ni 109, matundu ya vyoo pia tunahitaji 203 wakati tunayo 36 tu. 
"Kutokana na idadi hiyo kubwa, wanafunzi wanalazimika kusomea nje na wengine kuingia kwa awamu,” alisema.
 
Mwaka huu shule hiyo imeandikisha wanafunzi 1,022 wa darasa la kwanza idadi ambayo ni sawa na wanafunzi wa shule moja.
 Chanzo:Nipashe
 
 
Top