Rais John Magufuli amewateua mabalozi watatu wapya watakaoiwakilisha
Tanzania nchi za nje, wakiwamo Dk. Asha Rose Migiro na Mathias Chikawe,
ambao alishiriki nao kwenye mchakato wa urais ndani ya CCM.
Mbali na Chikawe ambaye jina lake lilikatwa kwenye hatua za awali
za mchakato huo, Dk. Migiro aliingia katika hatua ya tatu bora sambamba
na Balozi Amina Salum Ali, ambaye alishika nafasi ya pili.
Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais
Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema mwingine aliyeteuliwa kuwa Balozi ni Dk.
Ramadhan Dau, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mkuu wa Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Msigwa ambaye kwenye taarifa yake alikuwa akimnukuu Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema vituo vya kazi vya mabalozi hao
vitajulikana baada ya taratibu husika za kidiplomasia kukamilika.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliagiza kurudishwa nyumbani kwa
mabalozi Dk. Batilda Buriani (Japan), Dk. James Msekela (Italia) na
Peter Kalaghe (Uingereza).
Sababu za kurejeshwa kwao, kwa mujibu wa Balozi Sefue, ni mabalozi
hao na watano kutofanya kazi kikamilifu ya kuiwakilisha nchi kama
majukumu yao yanaavyoeleza. Dk. Msekela ilielezwa kuwa mkataba wake
ulikuwa umemalizika.
Kutokana na hatua hiyo, vituo vilivyo wazi, ni na Brussels
(Ubelgiji) na Kuala Lumpur (Malaysia) baada ya Dk. Diodorus Kamala,
kuchaguliwa kuwa mbunge wa Nkenge mkoani Kagera. Kituo cha Kuala Lumpur
kiko wazi baada ya Dk. Aziz Mlima kuteuliwa kuwa katibu Mkuu wa Wizara
ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa
na Brasilia (Brazil) kutokana na Francis Malambugi kustaafu.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Dk. Magufuli kufanya uteuzi wa
mabalozi. Mara ya kwanza ulikuwa uteuzi wa Mahadhi Juma Maalim kuwa
Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, baada ya serikali kufungua ofisi ya
ubalozi katika nchi hiyo rafiki.
WASIFU WA MABALOZI WAPYA
Dk.Asha Rose Migiro
Aliwahi kuwa mhadhiri mwandamizi wa sheria katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam hadi mwaka 2000 alipoingia kwenye siasa na akawa mbunge na
baadaye kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto hadi mwaka
2005.
Mwaka 2006 hadi 2007 aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo
tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.
Mwaka 2007, aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa (UN),
Ban-Ki-Moon kuwa Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo, akiwa mwanamke wa pili
kushika nafasi hiyo, ambayo aliishika hadi mwaka 2012 mkataba wake
ulipomalizika.
Mwaka 2013, Dk. Migoro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania (OUT) na baadaye kuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Baadaye aliteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa katiba na Sheria na Katiba
hadi Oktoba, mwaka jana.
Dk. Ramadhani Dau
Aliwahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya TAN-RE, mjumbe wa bodi ya hoteli
ya Serena, benki ya Barclays, Benki Kuu ya Tanzania na Jubilee
Insurance.
Pia aliwahi kuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitivo
cha Biashara Idara ya Masoko; Mkurugenzi wa Masoko wa iliyokuwa Mamlaka
ya Bandari Tanzania (THA) sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania
(TPA).
Mathias Chikawe
Alianza utumishi wa umma Aprili, 1975 akiwa Mwanasheria wa Serekali
Daraja la Tatu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serekali, mwaka 1976
– 1985 alikuwa Mshauri wa Sheria, Wizara ya Kilimo na Mifugo, mwaka
1985 hadi 1988 Ofisa Utumishi Mwandamizi, Idara ya Kanuni za Utumishi
Serikalini – Ofisi ya Rais (Utumishi).
Mwaka 1988 hadi 1998 aliwahi kuwa Ofisa Utumishi Mkuu na baadaye
Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DAP) kufikia Mkurugenzi wa Huduma za
Ikulu, Ofisi ya Rais – IKULU na mwaka 1998 hadi 2005 aliwahi kuwa Katibu
Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT).
Mwaka mwaka 2005 hadi 2015 alikuwa Mbunge wa Nachingwea mkoani
Lindi na kushika nafasi za Naibu Waziri wa katiba na Sheria (2006 na
2008); Waziri katika wizara za Katiba na Sheria (2008 – 2010); Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora (2010- 2012), Kariba na Sheria (2012
-2014) na Mambo ya ndani ya nchi (2014- 2015).
WARITHI WA CHAGONJA, KOVA WATEULIWA
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amempandisha cheo aliyekuwa
Naibu Kamishna wa Polisi Simon Sirro kuwa Kamishna wa Polisi na kumteua
kuwa Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, kujaza nafasi
iliyoachwa wazi na Suleiman Kova.
Taarifa hiyo pia ilisema Naibu Kamishna wa Polisi Albert
Nyamuhanga, amepandishwa kuwa Kamishna wa Polisi na ameteuliwa kuongoza
Idara ya Fedha, Utawala na Lojistiki. Anajaza nafasi iliyoachwa wazi na
Kamishna Clodwing Mathew Mtweve, aliyeteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa
wa Mwanza.
Pia Naibu Kamishna wa Polisi Robert Boaz, amepandishwa cheo kuwa
Kamishna na ameteuliwa kuongoza Idara ya Intelijensia kujaza nafasi
iliyoachwa wazi na Kamishna Valentino Mlowola aliyeteuliwa kuwa Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kamishna Msaidizi Mwandamizi Nsato Marijani Mssanzya ambaye
amepandishwa cheo kuwa Kamishna wa Polisi, ameteuliwa kuongoza Idara ya
Mafunzo na Operesheni, iliyokuwa chini ya Paul Chagonja, aliyeteuliwa
kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi.
Wakati huo huo, Rais Dk. Magufuli amemteua Dk. Modestus Kipilimba
kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
“Kabla ya Uteuzi huu, Dk Kipilimba alikuwa Mkurugenzi wa
Menejimenti ya Udhibiti katika Benki Kuu ya Tanzania. Dk. Kipilimba
anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Dickson Maimu, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa,” ilisema taarifa hiyo.