SERIKALI mkoani Kilimanjaro imeagiza kusimamishwa kazi mara moja maofisa wanne kutoka Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa madai ya kuchochea kuwapo kwa migogoro ya ardhi, matumizi ya vitabu bandia vya risiti na utendaji mbovu.
Kadhalika serikali imemtaka Katibu Tawala wa mkoa huo, Severine Kahitwa, kuwarejesha wilayani hapa watumishi wawili wa idara hiyo ambao wamehamishiwa katika wilaya za Siha na Mwanga ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla baada ya kusikiliza kero na migogoro ya ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Holili Wilaya ya Rombo ambako alijiridhisha kuwa maofisa hao wanahusika.
“Mkurugenzi fuata sheria zilizopo, hakikisha leo hii (jana) watumishi hao wanaandikiwa barua za kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi yao na wewe Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mnipe taarifa ndani ya siku 14 kuhusu mazingira ya rushwa,” alisema Makalla.   
Maofisa hao akiwamo Ofisa Ardhi wa Wilaya, Jovin Mtei na wengine watatu kutoka Idara ya Upimaji wa Viwanja wamedaiwa kuwa tatizo huku pia wakidaiwa kuuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wawili.
Mkuu wa mkoa aliwataja maofisa wengine wanaotakiwa kusimamishwa kuwa ni Mkuu wa Idara, Ardhi, Maliasili na Mazingira, Arbogast Mhumba; Mpimaji Ardhi Msaidizi, Mipawa Richard na mwingine Bartholomew Urassa.
Makalla pia aliwataja watumishi ambao Katibu Tawala Mkoa anatakiwa awarejeshe wilayani hapa kuwa ni Ofisa Mipango Miji Wilaya ya Siha, John Mpanju na Mpimaji wa Ardhi Msaidizi Wilaya ya Mwanga, Ulomi A ambao kwa nyakati tofauti walifanya makosa mbalimbali wakiwa watumishi wa Wilaya ya Rombo.
 
Top