WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameagiza
mameneja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), watakaoshindwa kutekeleza
maagizo ya wizara hiyo, waondolewe kazini ifikapo Machi mosi mwaka huu.
Alisema hayo jana wakati wa kikao chake na watendaji wa Tanesco na
taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo, kilichofanyika katika
kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alitaja maagizo hayo kuwa ni kuunganisha huduma kwa
wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya ankara za umeme, kupunguza
manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa
mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, ifikapo Machi mosi mwaka huu
atatuthibitishia kama mameneja hawa wataendelea na majukumu haya
wanayosimamia ama la, na hii itatokana na ufanisi wa utendaji katika
majukumu tuliyowapangia,” alisema Profesa Muhongo.
Mbali na mameneja hao, Profesa Muhongo ameagiza Kitengo cha Uwekezaji
cha Tanesco, kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme ifikapo Aprili 2
mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo waondolewe katika nafasi hiyo kwa
kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Hapa hatuna mzaha kwani mahitaji ya umeme ni makubwa na tuna miradi
mingi ya usambazaji umeme kwa wananchi ikiwemo miradi ya Rea (Wakala wa
Umeme Vijijini). “Wananchi wanahitaji umeme kwa matumizi ya majumbani na
kuanzisha viwanda vidogo, sasa bila miradi mipya ya umeme, tutashindwa
kusambaza umeme kwa wananchi hawa kwa kuwa kiasi cha umeme tulichokuwa
nacho sasa bado hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo pia aliwaasa mameneja wa Tanesco wa Kanda,
kukaribisha wawekezaji mbalimbali wa umeme ikiwemo miradi midogo ya
uzalishaji umeme wa maji, ili nchi iwe na umeme wa kutosha badala ya
kuwakatisha tamaa wawekezaji hao.
Alionya watumishi watakaoleta urasimu katika kujadili masuala ya
uwekezaji wa nishati, wataachia ngazi kwani ndio wanaokwamisha juhudi za
Serikali katika kuongeza kiasi cha umeme nchini.
“Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji)
kwa sasa pale anapojitokeza mwekezaji wa miradi ya umeme, lazima
mjadiliane naye kwa pamoja badala ya mwekezaji husika kwenda Tanesco na
baadaye Ewura au TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli). “Hivyo
mwekezaji anapokuja, jadilini naye kwa pamoja ili msitumie muda mrefu
katika utekelezaji wa suala moja na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa
miradi mbalimbali,” alisema Profesa Muhongo.
Pia amewaagiza watendaji wa TANESCO katika vitengo vya ukaguzi,
kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa ikiwemo usimamizi madhubuti wa
nguzo za umeme, ambazo baadhi huanguka kila inapofika msimu wa mvua na
kusema kuwa suala hilo halikubaliki.
Hatua hiyo ya Profesa Muhongo, imelenga kutekeleza malengo ya Wizara
hiyo kuhakikisha asilimia 67 ya vijiji vyote nchini, vitapata umeme
katika miaka miwili na nusu ijayo. Mbali na kuunganisha watu wengi na
huduma hiyo, juhudi kuongeza uzalishaji wa umeme, Profesa Muhongo
alizieleza mara tu alipoapishwa kushika wadhifa huo Desemba mwaka jana.
Katika hafla hiyo, Profesa Muhongo alisema Tanzania ina vyanzo vingi
vya kuzalisha umeme, lakini bado umeme unaozalishwa hautoshi na kuwataka
wawekezaji wenye uwezo watumie fursa hiyo kuwekeza katika sekta hiyo.
Aidha alisisitiza kuwa ili Taifa lifanikiwe kuwa nchi yenye kipato
cha kati kufikia mwaka 2025, ni lazima nchi iwe na umeme wa kutosha,
hivyo hadi kufikia mwaka huo, uzalishaji wa umeme unapaswa kufikia
megawati 10,000