IDARA ya Uvuvi na Mifugo, Hamashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa imekamata shehena ya samaki wabichi na wakavu wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20.
Shehena hiyo ya samaki inadaiwa kuvuliwa kwa kutumia nyavu haramu za
kuvulia samaki ambazo zimepigwa marufuku kuvulia katika Ziwa Rukwa
wilayani Sumbawanga ambayo ilikuwa ikisafirishwa kwenda nchi jirani ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia mji mdogo wa Tunduma mkoani
Mbeya .
Akizungumza na chanzo chetu Ofisa Uvuvi na Mifugo wa Halmashauri ya
wilaya ya Sumbawanga , Denis Maghala alisema baadhi ya wavuvi
wanaendelea kuvua katika Ziwa Rukwa licha ya kufungwa kwake kwa miezi
mitatu hadi Machi 31 mwaka huu.
“Wavuvi hao wanavua ziwani kwa njia ya haramu na kuwauzia samaki
wabichi na wakavu kwa wafanyabiashara ambao husafirisha kwa kutumia
magari makubwa kwenda jijini Mbeya pia nchi jirani ya DRC,” alisema.
Alisema kuwa idara yake imekuwa ikifanya doria za mara kwa mara
ambapo Januari 29 mwaka huu gari aina ya Fuso lenye nambari za usajiri
T910 ARL mali ya Selemani Jimmy lilikamatwa likiwa na shehena ya samaki
wabichi na wakavu wenye thamani ya mamilioni.