“WAKATI Profesa Maghembe anateuliwa kuwa Waziri wa Maji, Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Kahama na Shinyanga ulikuwa unahudumia idadi ndogo sana ya wananchi wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga na ulikuwa unafanya kazi chini ya asilimia 15 ya uwezo wake, lakini baada ya kuteuliwa katika wizara hiyo, huduma ya maji kupitia mradi huo iliongezeka.
Waliobeza uteuzi wake katika Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni waziri mzigo hawajui uwezo wa Profesa Maghembe.” Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama– Shinyanga (KASHWASA), Clement Kivegalo. Kivegalo alitoa kauli hiyo hivi karibuni mjini Shinyanga alipokuwa akizungumzia Baraza la Mawaziri aliloliteua Rais John Magufuli.
Kwanza mhandisi huyo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuipitisha nchi hii katika uchaguzi salama na kupatikana chaguo la Watanzania ambalo ni Dk Magufuli. Anasema katika nchi yoyote duniani, wananchi huwa na matamanio ya kumpata kiongozi bora na atakayetekeleza kwa vitendo ahadi za chama chake na anayesukumwa na maslahi mapana ya nchi yake.
“Hivi sasa ikiwa ni miezi michache tu tangu Rais John Magufuli ashike hatamu za uongozi wa nchi yetu, wananchi walio wengi wanaonekana kuridhishwa na kasi ya utendaji wake na hususani baraza aliloliunda,” anasema. Anasema kwa mwenendo wa utendaji kazi wa Rais John Magufuli na Serikali yake, bila shaka utawezesha kurejesha uzalendo wa mtu mmoja mmoja hapa nchini, hali ambayo itaimarisha umoja, upendo na mshikamano wa wananchi.
Uteuzi wa Profesa Maghembe Anasema Desemba 23 mwaka 2015 Rais John Magufuli alikamilisha uteuzi wa Baraza la Mawaziri kwa kujaza wizara nne zilizokuwa zimeachwa kiporo na moja ya wizara hiyo ni ya Mali Asili na Utalii aliyopewa Profesa Jumanne Maghembe kuisimamia. Anasema, kama ilivyo ada, baadhi ya wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii walitoa maoni yao kuhusu uteuzi huo huku wengine wakielekeza kidole kwa Profesa Maghembe, wakishangaa ni kwa nini Rais alimteua kushika Wizara ya Mali Asili na Utalii ambayo ni moja ya wizara nyeti.
“Sisi tunaomjua Maghembe tulibaki tu kuwashangaa waliohoji uteuzi wake lakini tulifurahi na hata kama angelimrejesha kwenye wizara ya maji tungefurahi pia,” anasema Kivegalo. Anasema Profesa Maghembe kama ilivyo kwa binadamu wote, anaweza kuwa na mapungufu ya hapa na pale lakini kwa ujumla, anasema ni moja wa mawaziri wazalendo na wachapakazi.
Uwezo wa Maghembe Anasema katika kipindi alichosimamia sekta ya maji nchini, yeye binafsi ameshuhudia ongezeko la miradi ya maji katika maeneo ya mbalimbali nchini ambayo yamewezesha pia ongezeko la idadi ya wananchi wanaopata huduma ya uhakika ya maji safi na salama, mijini na vijijini. Anasema ipo mifano mingi juu ya utendaji kazi mzuri wa Profesa Maghembe, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Kahama na Shinyanga.
Anasema kupanuliwa kwa mradi huo ni moja ya juhudi zilizofanywa na Profesa Maghembe katika sekta ya maji, ambapo wakati anakabidhiwa wizara, mradi huo ulikuwa unahudumia idadi ndogo ya watu, sawa na asilimia 15 ya uwezo wake. “Ukiondoa miji ya Kahama na Shinyanga, kulikuwa na vijiji 39 tu vya wilaya za Misungwi, Kwimba, Shinyanga na Kahama vilivyokuwa vinapata huduma ya maji huku zaidi ya vijiji 40 vya wilaya hizo vilivyopo pembezoni mwa bomba linalosafisha maji vikiwa havina huduma ya maji,” anaeleza.
Anasema wakati Profesa Maghembe alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo wa maji mwaka juzi, alisikitishwa na hali ya wananchi wengi kukosa huduma ya maji ikizingatiwa kuwa mradi ulijengwa kwa gharama ya Sh bilioni 254, fedha za ndani zinazotokana na kodi za wananchi lakini ulikuwa hauwanufaishi wananchi wengi. “Miezi michache baada ya ziara hiyo, uliibuliwa mradi wa maji uliounganisha vijiji hivyo 40 na ndani ya mwaka mmoja vijiji 16 viliunganishwa kwenye mtandao wa maji ya Ziwa Victoria,” anasema.
Anasema mji wa Ngudu ulioko Kwimba mkoani Mwanza uliunganishwa pia kwenye mtandao huo na kwamba Kuunganishwa kwa mji wa Ngudu na vijiji 16 kwenye mtandao huo, kuliwezesha wananchi zaidi ya 91,113 pamoja na mifugo yao kupata huduma ya uhakika ya maji ya uhakika. Anasema, katika mkoa wa Shinyanga, Profesa Maghembe ameondoka Wizara ya Maji akiwa ameacha mradi wa kuunganisha vijiji vingine 24 ukiendelea pamoja na mradi mwingine wa kuunganisha Mji wa Kishapu.
“Halikadhalika, miezi michache ijayo, utaanza mradi wa kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Manispaa ya Tabora na miji midogo ya Igunga, Nzega, Kagongwa, Isaka na Tinde. “Kuibuliwa kwa mradi huu mkubwa, ambao utagharimu zaidi ya Sh bilioni 200, kumetokana na dhamira ya Maghembe na Serikali katika kuhakikisha inawaondolea wananchi kero ya maji,” anasema.
Anasema bila shaka, mwananchi aliyeguswa na mafanikio hayo anaposikia Profesa Maghembe akiitwa waziri mzigo ataishia kushangaa tu. “Nimesema haya kuhusu utendaji kazi wa Profesa Maghembe kwa eneo dogo tu ikilinganishwa na maeneo mengi ambayo kazi kubwa imefanyika chini ya uongozi wake,” anasema.
Anasema ndio maana yeye na wengine waliofanya kazi kwa karibu na Magh1 embe hawakushangaa waliposikia katika tathmini iliyofanywa na Ofisi ya Rais Kitengo kinachosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), sekta ya maji ikatajwa kuongoza.
Anasema pamoja na mafanikio hayo makubwa, bado ipo changamoto kubwa ya kuwapatia wananchi wengi zaidi huduma ya maji. Anakiri kwamba baadhi ya wananchi walikuwa hawaridhishwi na kasi ya serikali iliyopita katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji, lakini hali hiyo haitokani na udhaifu wa Profesa Maghembe bali ufinyu wa bajeti.
Anasema sifa nyingine ya utendaji aliyoiona kwa Profesa Maghembe ambayo kwa kiasi kikubwa inaendana na mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Tano, ni msisitizo wake juu ya matumizi ya watalaamu wa ndani katika ujenzi wa miradi ili kupunguza gharama.
Anasema msisitizo huo ndio uliowezesha mradi wa kufikisha maji katika mji wa Ngudu kujengwa ndani ya miezi mitatu ambao, pamoja na mambo mengine, ulijumuisha ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilometa 50 na ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa gharama ya takribani Sh bilioni 2.4 tu.
Anasema hatua hiyo iliokoa zaidi ya Sh bilioni 8 ambazo zingetumika endapo mradi ungepembuliwa, ukasanifiwa na kujengwa kwa kutumia kampuni binafsi ya nje. “Halikadhalika fedha ambayo ingetumika kuunganisha vijiji saba kwenye mtandao wa maji wa Ziwa Victoria endapo makampuni binafsi yangetumiwa, ndiyo iliyotosha kuunganisha vijiji 16 kupata huduma ya maji kwa kuwatumia wataalamu wa ndani,” anasema
 Chanzo: HabariLeo

 
Top