MKAZI wa Kata ya Igurubi, wilayani Igunga mkoani Tabora, Shabani Khamisi (18), amehukumiwa kwenda jela miaka 30 na kulipa faini ya Sh laki tatu, baada ya Mahakama ya Wilaya kumtia hatiani kwa kosa la kulawiti mwanafunzi wa darasa la pili.
Akitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Hakimu wa Mahakama hiyo, Leonard Nkola alisema adhabu hiyo imetolewa kutokana na vitendo vya ubakaji kuongezeka katika maeneo mbalimbali nchini, huku wahusika wakijua kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Hakimu Nkola alisema ameridhika na ushahidi wa mashahidi sita wa upande wa mashitaka na Mahakama imeona mshitakiwa anastahili adhabu hiyo.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Frank Matiku aliiambia mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 24, mwaka jana saa sita mchana katika Kata ya Igurubi.
Mwendesha Mashtaka alidai mshitakiwa alimkamata mwanafunzi huyo wa darasa la pili mwenye umri wa miaka 10, katika Shule ya Msingi Igurubi na kumvutia kichakani na kumlawiti na kumsababishia maumivu makali.
 
Top