Siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuahidi kuwa serikali yake imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi ya Lipa Kadiri Unavyopata (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi tisa, baadhi ya vyama vya wafanyakazi vimepokea kwa furaha.
 
Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama mbalimbali vya wafanyakazi walisema kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza matatizo mbalimbali yanayowakabili wafanyakazi.
 
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema Rais Magufuli anawarudishia furaha wafanyakazi iliyotoweka miaka ya nyuma.
 
Mukoba alisema walimu walilia kwa muda mrefu toka utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, hivyo kitendo cha Rais Magufuli kuwakumbuka, ni jambo la maana.
 
“Rais Magufuli anataka kufanya mambo ambayo walimu na wafanyakazi walikuwa wanalia kwa muda mrefu, hivyo kutaleta neema kubwa kwa wafanyakazi kote nchini,” alisema Mukoba.
 
Aliongeza kupunguza kodi hadi kufikia asilimia tisa, kutawasaidia wafanyakazi wa mishahara midogo, lakini haitawasaidia wafanyakazi wa mishahara mikubwa.
 
Alisema CWT ina imani na Rais Magufuli katika kutekeleza ahadi zake kwa kuwa ameanza kwa kasi kubwa.
 
Naye Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya, alisema shirikisho hilo limepokea kwa furaha na wanasubiri utekelezaji wake.
 
Mgaya alisema kodi kupunguzwa hadi kufikia asilimia tisa, ni kilio kilichokuwa kinapigiwa kelele kwa muda mrefu na wafanyakazi wengi nchini.
 
Aliongeza kuwa serikali ya Rais Magufuli ni ya utekelezaji zaidi, hivyo wana imani kuwa ahadi hiyo itatekelezwa.
 
Juzi, Rais Magufuli akiwa kijijini kwake Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, alitoa ahadi hiyo ya kushusha makato ya kodi kwa wafanyakazi kwa kuwa kilio hicho kimekuwa kikisikika tangu miaka ya nyuma.

Chanzo: Nipashe

 
Top