WATU watano wamekufa na wengine sita kujeruhiwa vibaya baada ya
kuangukiwa na mwamba wa mawe katika shimo la mgodi mkubwa wa zamani wa
Resolute wilayani hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Khamis Selemani amethibitisha tukio
hilo na kuwataka wachimbaji kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki
cha masika, kwani ardhi imelowa maji.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla amethibitisha na
kuzungumzia tukio hilo, akisema lilitokea jana saa saba mchana baada ya
kundi la wachimbaji wadogo wa mgodi wa umoja kuvamia eneo hilo ambalo
limepigwa marufuku na serikali kutokana na kuwa hatarishi.
Alisema licha ya zuio hilo, baadhi ya wachimbaji wamekuwa wakiingia kwa kificho kuchimba hali iliyosababisha maafa hayo.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na Joseph Mpenda, mkazi
wa Shinyanga, Mohamed Mohamed ambaye ni mkazi wa Singida, Manona Nyombi
mkazi wa Bariadi na Modesta Leonard mkazi wa Nzega na mmoja hakuweza
kutambulika .
Majeruhi ni Kangwa Mayenga (22) mkazi wa Bariadi, Agnes Anthony (40)
mkazi wa Chato, Deus Alphonce (45) mkazi wa Igunga pamoja na Mathias
Mapunda mkazi wa Chato na kuongeza kuwa, wanaendelea kutibiwa. Majina ya
majeruhi wawili hayakupatikana na bado hawawezi kuzungumza.