JESHI la polisi wilayani Arumeru Mkoani Arusha, jana asubuhi lilisambaratisha kikundi cha watu waliokuwa wakifanya maandalizi ya mkutano wa hadhara wa ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Matevesi wilayani humo.


Mkutano huo ulidaiwa kuwa ulikuwa uhudhuriwe na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowasa.
Polisi walichukua hatua hiyo baada ya wafuasi wa chama hicho, kulazimisha kufanyia mkutano huo katika eneo ambalo haliko katika ratiba.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Januari 7 mwaka huu chama hicho kinapaswa kufanya mkutano wake katika eneo la Ematasia.
Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba ujenzi wa jukwaa na maandalizi mengine, yalionekana kufanyika eneo la Kisongo sokoni, karibu na Ofisi za Chama Cha Mapinduzi(CCM) Kata ya Matevesi.
Inaelezwa ukiukwaji wa ratiba hiyo, uliofanywa na chama hicho umetokana na taarifa za ghafla kuwa Lowasa angehudhuria mkutano huo bila kufahamu kuwa ratiba ya jana, ulikuwa ufanyike nje ya mji ya Kisongo katika eneo la Ematasia.
Baada ya kufahamika kuwa eneo la mkutano ni nje ya Kisongo, viongozi wa juu wa Chadema bado walikuwa wakishinikiza kwamba ni lazima mkutano ufanyike eneo hilo la mjini Kisongo, kwa kuwa Lowassa asingeweza kupelekwa katika mkutano ambao unafanyia eneo la porini kidogo, nje ya mji wa Kisongo.
Inaelezwa pia sababu nyingine ya kulazimisha mkutano katika eneo hilo ni hofu ya kukosa watu katika mkutano huo, kama ilivyotokea katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika Kata ya Ngarenanyuki.
Kufuatia hali hiyo, polisi ilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema. Ghafla kikosi cha polisi cha kutuliza ghasia (FFU) kilifika na kuwaamuru wafuasi hao wa Chadema, waliokuwa wakifanya maandalizi, kusitisha mara moja na kung’oa kila kitu na kufuata ratiba inavyoelekeza.
Kutokana na amri hiyo, wafuasi hao walitii amri hiyo ya polisi, ambapo walianza kuondoa mapambo, bendera na vitambaa vyenye nembo za chama chao, zilizokuwa zikipamba jukwaa kuu na kupakia katika gari na kuondoka, wakisindikizwa na gari la polisi na huku wakizomewa na watu waliokuwepo katika eneo hilo la soko.
Mbali na chama hicho kulazimishia ratiba hiyo, pia kulikuwa na hatari nyingine ya kuibuka kwa mapigano baina ya wafuasi wa CCM na Chadema, kwa kuwa siku hiyo wafuasi wa CCM walikuwepo kwa wingi katika eneo hilo, kwa kuwa walikuwa wakijiandaa kwenda katika mkutano wa hadhara wa kampeni katika eneo la Lemuguru.
Chanzo HabariLeo

MATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFY HAPA>>
 
Top