Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi, Damas Nyanda
WAANDISHI wa habari, viongozi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) akiwemo
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Katavi wamenusurika kifo, baada ya gari
walilokuwa wakisafiria, kuacha njia kisha kuparamia mti msituni.
Ajali hiyo ilitokea wakati wakitoka kwenye uzinduzi wa kampeni ya
uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Kasansa wilayani Mlele.
Mashuhuda ajali hiyo, walidai ilitokea Januari 6 saa 3 usiku katika
eneo la Sikitiko ndani Hifadhi ya Taifa ya Katavi katika barabara ya
Mpanda mjini kwenda Mpimbwe wilayani Tanganyika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damasi Nyanda alisema kuwa ajali
hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser, mali ya CCM wilaya ya
Mpanda, namba T 604 TEU, iliyokuwa ikiendeshwa na Charles Emmanuel
(54), mkazi wa Mtaa wa Makanyagioa Manispaa ya Mpanda .
Walionusurika kifo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Mselem
Abdallah, Katibu Mwenezi wa Mkoa wa CCM, Joseph Makumbule na Mjumbe wa
Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa, Jeneroza Mmbamba.
Waandishi wa habari walionusurika kifo ni Ernest Kibada wa Adam TV na
Walter Mguluchuma, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa
Habari Mkoa wa Katavi.
Alipohojiwa, Mguluchuma alisema ajali hiyo ilitokea wakati wakitokea
kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kasansa,
ambapo CCM walizindua kampeni zao .
Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kasansa, utafanyika kufuatia
kifo cha Sissto Cherehani aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya
CCM. Uchaguzi huo utafanyika Januari 22 , mwaka huu.
Naye Kibada alisema kuwa dereva wa gari hilo, alishindwa kulimudu
baada ya usukani wa gari hilo kukatika, hivyo liliacha njia na kuingia
msituni kisha kuparamia mti. Alisema kuwa askari wa hifadhi ya taifa ya
Katavi, walifika eneo hilo la tukio baada ya kupita saa mbili na kutoa
msaada wa usafiri .
Chanzo: HABARI LEO