Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projestus Rwegasira
SERIKALI kupitia kitengo maalum cha uchunguzi wa jinai ya kimtandao,
imefanikiwa kukamata watuhumiwa 690 kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa
mtandao.
Watuhumiwa hao ni matapeli, wezi, waporaji wa simu za mkononi na
wengineo wanaotumia mfumo wa intaneti kuibia watu wasiokuwa na hatia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projestus
Rwegasira alisema juzi jioni kuwa ofisi yake imekuwa ikikabiliana
kikamilifu na wahalifu hao.
Alisitiza kwamba wahusika wote wa vitendo hivyo, watakamatwa. Meja
Jenerali Rwegasira alikuwa akizungumza katika mahojiano katika kipindi
cha Tunatekeleza, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa(TBC). Kwamba
wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vya serikali, inaandaa mashtaka
dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa na watafikishwa mahakamani.
“Tunafanya kila juhudi kuzuia vitendo vya uhalifu wa kimtandao,
tayari tumekamata baadhi ya watuhumiwa na watakabiliana na mkono wa
sheria mahakamani,” alisema.
Alisema serikali imeunda kitengo maalumu chini ya Wizara ya Mambo ya
Ndani, kukabiliana na udanganyifu na uhalifu wa kimtandao nchini na
kimekuwa kikifanya kazi nzuri.
Rwegasira alisema, “Ningependa kuutangazia umma kuwa huru kutoa
taarifa ya vitendo kama hivyo polisi mara wanapoona, tuna uwezo wa
kufuatilia simu zilizoibwa na kuwakamata watuhumiwa”.
Mwezi Januari mwaka huu, Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Veronica Sudayi alisema tangu
kupitishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na Miamala ya Kielektroniki
ya 2015 mwezi Septemba 2015, kiwango cha wizi na udanganyifu nchini,
kimepungua kwa asilimia 60.
Sudayi alisema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuhusu Sheria hiyo ya Makosa
ya Mtandao. Kuhusu amani na usalama, katibu mkuu huyo alisema serikali
imejiandaa vya kutosha kulinda watu na mali zao na kujipanga vya
kutosha.
Alisema jeshi la polisi liliweza kukabiliana na changamoto za
kiusalama katika mikoa ya Tanga na Mwanza baada ya watu wasiokuwa na
hatia kuuawa na majambazi. Alisema katika tukio la Tanga, watuhumiwa 28
walikamatwa na wengine nane walikamatwa kuhusiana na tukio la Mwanza.