suala la kudaiwa
kudanganya umri likiwa bado ‘bichii’, taarifa zinadai kuwa mshindi wa Miss
Tanzania 2014, Sitti Mtemvu ametoweka na hajulikani alipo, Risasi Mchanganyiko
limechimbua stori kamili.
Mshindi wa Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu
Shughuli ya kumsaka mrembo huyo ili kujua undani wa sakata
lake ilianzia Temeke ambako ilielezwa kuwa ndiko anakoishi.
Mapaparazi wetu walipofika katika nyumba waliyoelekezwa,
walikuta imebadilishwa na kuwa Ofisi ya Vikoba ambapo mmoja wa wahudumu wa
ofisi hiyo kwa sharti la kutoanika jina lake gazetini, aliwataka waandishi wetu
kwenda Mbezi-Makonde akidai ndiko anakoishi kwa sasa.
“Hapa ilikuwa nyumba ya zamani lakini kwa sasa ni ofisi na
Sitti hakai hapa, kama mnamtaka nendeni Mbezi-Makonde huko nasikia ndiko
anakoishi,” alisema mtumishi huyo.
Mapaparazi wetu hawakuchoka, walifunga safari hadi
Mbezi-Makonde ambapo walikuta nyumba yenye maduka yaliyoandikwa Mtemvu
Foundation, wakaenda moja kwa moja katika saluni mojawapo iliyokuwa na bango
lililosomeka Malisa huku likiwa na picha ya Sitti sambamba na namba za simu.
Sitti Mtemvu wakati wa kutwaa taji la Miss Tanzania 2014
Dada mmoja aliyeonekana kufanana na Sitti alizidi kutibua hali ya
hewa baada ya kusema Sitti amesafiri nje ya nchi pasipo kufafanua nchi
gani.“Sitti amesafiri nje ya nchi, ila kama mnamtaka nafikiri nitawapa
namba zake akirudi kati ya Jumatatu au Jumatano ya wiki ijayo (wiki
hii),” alisema dada huyo pasipo kutaja jina lake.
Mmoja wa majirani wa mrembo huyo alihoji inawezekanaje mrembo huyo
akasafiri nje ya nchi wakati suala lake la umri halijapata ufumbuzi?“Mh!
Ataondokaje wakati bado ana majanga ya umri?” alihoji jirani huyo.
Aidha, mapaparazi wetu hawakutaka kuishia
hapo, Jumapili iliyopita walitia timu Buza Kipera katika Kanisa la The
Revelation Church la Nabii Yaspi Bendera ambalo ilielezwa kuwa Sitti
anaabudu, ili kujiridhisha kama yupo, lakini pia hakuonekana huku
waumini wakidai hawajamuona kwa siku za karibuni.
Nabii Yaspi Bendera wa Kanisa la
The Revelation Church.
“Hatumuoni siku hizi, ila alikuwa anakuja katika ibada ya
peke yake kwa nabii saa kumi lakini siku za karibuni hatumuoni,” alisema
muumini mmoja.Katika ibada inayoendeshwa kanisani hapo ambayo mapaparazi wetu
walizama ‘kiintelijensia’, Nabii Yaspi alisikika akimkingia kifua Sitti kuwa
alistahili ushindi na kumtabiria kufika mbali na hata kuwa Miss World huku
akiwaonya wanaomfuatilia mrembo huyo.
“Mara ya kwanza nilimtabiria Sitti kushinda u-miss Tanzania
na kweli akashinda, sasa wanatokea watu wakidai mara ana hipsi kubwa, ooh
kadanganya umri, huu wote ni upepo tu na utapita.“Kama Sitti hatakengeuka
kwenye imani yake atafika mbali zaidi na kushinda hata Miss World. Wale wote
watakaoendelea kumfuatilia wataparalaizi,” alisema Nabii Yaspi.
Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, Wakala wa Usajili, Ufilisi
na Udhamini (RITA), walisema bado wanalifanyia uchunguzi suala la Ritta kudaiwa
kufoji cheti cha kuzaliwa kutokana na baadhi ya nyaraka zake kuonesha amezaliwa
mwaka 1989 huku yeye akidai amezaliwa 1991.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk.
Fenella Mukangara akitafakari jambo.
Wakati RITA na BASATA wakiwa hawajatoa tamko lolote
kufuatia uchunguzi waliodai wataufanya, gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara ili
azungumzie sakata hilo.
“Waziri ni mtu mkubwa sana kuzungumzia suala kama hilo,
watafute wasaidizi wangu pale wizarani watakuambia kinachoendelea. Naweza kutoa
tamko halafu nikaonekana mtu wa ajabu, kumbe watu wanaendelea kulifanyia kazi,
nenda kamuone Mkurugenzi wa Utamaduni atakusaidia,” alisema Waziri huyo
alipozungumza nasi kwa njia ya simu.