Wakati Chama cha mapinduzi kikielekea katika hatua ya kuteua mgombea Urais wa chama hicho, Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, amefyatuka na kusema Urais ni hatima ya Watanzania hivyo lisifanywe mchezo kuwa mtu yeyote anaweza kuucheza.

Amesema si vizuri watu waliopewa vyeo ndani ya CCM kuendelea kukitumia chama kwa mambo yao binafsi.

"Kama wana mashaka chama hiki kina historia, vyema wakatutafuta watu ambao tupo, watu tunaojua mambo ya chama," alisema.

Alisema wanaofanya jitihada za kuunda mazingira ya kukitafutia chama kushindwa, wanataka historia ya CCM iishie katika awamu ya nne.

Kingunge ambaye alikuwa miongoni mwa wanachama waliomdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, katika Wilaya ya Kinondoni, alisema yupo ndani ya chama hicho kwa miaka 60 sasa, ameona mengi ya mkoloni na Tanzania.

"Asilimia kubwa ya Watanzania ni maskini na chama chetu tangu mwanzo tulisema tutapambana na umasikini...Pamoja na mambo mazuri yaliyofanywa lakini sio mwisho, tunahitaji uongozi utakaotutoa katika umaskini na linawezekana hilo," alisema Kingunge.

Alisema ni mwiko kumhukumu mtu kabla ya vikao kwani haijawahi kufanywa hivyo mwaka 1995 na 2005, na hawatafanya hivyo mwaka huu
"Wakifanya hivyo tutakataa, tunataka mchakato ufuate taratibu zilizowekwa, nimemsikia kiongozi wetu mmoja alizungumzia katika Tv kuwa mtu hawezi kwenda kujinadi yeye binafsi bali chama ndio kinamnadi...Mimi nataka niseme kuna ngazi mbili; mwanachama anatakiwa kujinadi ndani ya chama na ndiyo tumefanya hivyo miaka yote kwa mujibu wa taratibu na ndivyo wanavyofanya kina Lowassa, anajinadi kwa wanachama," alisema.

Alisema baada ya mkutano mkuu wa kumpata mgombea, atanadiwa na chama hivyo si vizuri watu waliopewa vyeo kutumia chama kwa mambo yao binafsi.

"Katika utaratibu wetu tuna misingi ya kuamua na mwenyekiti wa chama chetu, Jakaya Kikwete, alitangaza yeye mwenyewe kwamba tutafute mgombea anayekubalika ndani na nje ya chama na ndio msimamo wa chama...CCM inamtafuta mtu anayekubalika ili kuleta ushindi ndani ya chama, wale wanaojitahidi kufanya hivyo kukitafutia chama kushindwa wanataka historia ya Chama Cha Mapinduzi iishie katika awamu ya nne," alitahadharisha.

Alisema suala la urais  lisifanyiwe mizengwe,  watu waulizwe wanamtaka nani na nani  atakayewatatulia changamoto zao.

"Watu wenye busara wanafuatilia mambo yanavyoenda na wameona, wagombea wapo wengi, wenye macho wapo wengi na wanaona, hivyo watu watulize vichwa na kuamua ni nani watamchagua," alisema Kingunge.

Naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa huo, Hemed Mkali, alisema Lowassa ndiyo Rais kwani anakubalika na wananchi wengi hivyo ni vyema viongozi wakaliangalia hilo.

"Kama wakipeleka kiatu cha polisi hawatakichagua hivyo CCM ikipeleka kiongozi ambaye hakubaliki watambue wananchi watamkataa,"alisema Mkali.
 
Top