Serikali ya Marekani imekunjua makucha kwa Tanzania kwa kuitaka kumaliza haraka mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, vinginevyo upo uwezekano wa kusitishwa msaada wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 472 (Sh. bilioni 999.4), za awamu ya pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya Milenia (MCC) la nchi hiyo.
Hatua hiyo inaonekana kuwa ni mtihani wa kwanza kwa Rais wa serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, ambaye tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka huu, anachapa kazi na matunda yake yanaonekana kwa umma wa Watanzania.
Kadhalika, Marekani imetaka kupata ufafanuzi wa watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya mtandaoni, wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Chanzo kimoja kimeieleza hivi karibuni, kuwa kuna maelekezo ya kutoka MCC, ambayo huenda yakasababisha kufutwa kwa msaada huo, iwapo mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hautatatuliwa kutotolewa ufafanuzi wa sheria ya makosa ya mtandaoni kabla ya kikao cha Bodi ya MCC Disemba, mwaka huu.