Aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Joseph Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe kutokana na matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni tatu.

Hatua hiyo inafuatia taarifa iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu mikataba mibovu iliyosainiwa na mkurugenzi huyo mwaka jana. Moja ya mikataba hiyo ni ule wa Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), ambapo mkataba uliokuwa ukitekelezwa ulikuwa wa mwaka 2004 uliotoza kila basi shilingi 4,000 badala ya ule wa mwaka 2009 uliokuwa ukitoza kila basi shilingi 8,000.

Kwamujibu wa Makonda katika ofisi ya Mkurugenzi wa jiji, mkataba uliokuwepo ulikuwa wa mwaka 2004 wakati kwa mzabuni alikuwa na mkataba wa mwaka 2009. Kutokana na hali hiyo badala ya serikali kupokea shilingi 8,000 kwa kila basi, ilikuwa ikipokea shilingi 4,000 na nyingine ziliishia katika mfuko wa mkurugenzi huyo.

Ukichukua shilingi 4,000 kwa kila basi ukazidisha kwa babasi 400 utajua kuwa kwa siku serikali ilipata hasara ya shilingi milioni 1.6 na ukizidisha kwa siku 30 utajua kuwa kwa mwezi serikali imepata hasara ya shilingi milioni 48.

Kutokana na hali hiyo kwa mwaka mzima serikali imepoteza kiasi cha shilingi milioni 576 ambapo ndani ya miaka mitano iliyopita serikali imepoteza kiasi cha shilingi bilioni 2.9.

 
Top