Kocha, Zdravko Logarusic akiwapa maelekezo wachezaji wa
Simba kabla ya kutimuliwa
In Summary:
SIMBA ilimpa kocha, Zdravko Logarusic, mkataba wa mwaka mmoja wiki tatu
zilizopita. Lakini juzi Jumapili ilifanya uamuzi mgumu kwa kumpiga chini kwa
maelezo kwamba haendani na hali halisi ya klabu.
Kabla ya kumtimua Logarusic, uongozi wa klabu hiyo ulipiga hesabu kali.
Kocha huyo alichukua Dola 24,000 (Sh 39.7milioni) ambazo ni ada ya kusaini
mkataba na ili kuuvunja mkataba anatakiwa alipwe Dola 5,000 (Sh8.1 milioni).
Viongozi hao wakaona ni bora kupoteza Sh 47.8 milioni kuliko kuangamiza
kiasi cha Sh3 bilioni na kuambulia patupu kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Simba imepanga kutumia bilioni hizo msimu ujao, ni fedha nyingi, zinawauma
viongozi wa klabu hiyo na ni dhahiri kuwa wanataka timu yao ifanye vizuri baada
ya kutumia fedha hizo na si kitu kingine. Tathmini hiyo ya hesabu ilionyesha
kuwa kocha Logarusic haendani na kasi yao, makosa yake yamekuwa ni yale yale
siku zote na amekuwa habadiliki. Wachezaji wanaonekana kumchoka hivyo kuokoa
jahazi, wakafanya maamuzi magumu.
Mwanaspoti ambayo ilikuwa ikifuatilia nyendo za kocha huyo kwa karibu tangu
ajiunge na klabu hiyo inakuletea sababu 10 zilizomwonyesha mlango wa kutokea;
Ukali uliopitiliza
Ukiwa katika uongozi sehemu yoyote unahitaji kuwa mkali kwa baadhi ya mambo,
lakini usisahau kutumia busara.
Logarusic alikuwa mkali, busara kwake ni kitu cha mwisho, mchezaji akikosea
kidogo alikua akijuta. Ukali wake ulipitiliza hadi baadhi ya wachezaji
waliogopa. Hali hiyo iliwachosha viongozi waliokuwa wakimwomba apunguze, japo
hakuwasikiliza.
Kulazimisha mambo
Kocha Logarusic anaiamini akili yake kwa asilimia 100, ana amini kila
akifanyacho ni sahihi, ni mgumu kutekeleza maoni ya wengine. Imani hiyo
ilimfanya awe na tabia ya kulazimisha mambo. Tabia hiyo ilimfanya Loga kuwatema
wachezaji 12 kwenye kikosi chake, ni idadi kubwa ya wachezaji lakini
alilazimisha hadi yakatimia, Uhuru Selemani pekee ndiye aliyesalimika tena kwa
jitihada zake mwenyewe na za baadhi ya viongozi. Uongozi ukaona kuburuzwa.
Wachezaji wa Mbeya City
Kabla ya kwenda mapumzikoni kwao Croatia, Logarusic alipendekeza klabu hiyo
isajili wachezaji kadhaa kutoka Mbeya City wakiwamo Deus Kaseke, Saady Kipanga
na Anthony Matogolo. Aliporejea hakumkuta hata mmoja wao kikosini hapo,
akaanzisha varangati akitaka wasajiliwe.