Rais Jakaya Kikwete amewaaga Marais wenzake wa umoja wa Afrika na kusema kuwa siasa ya nchi za nje na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano ya Tanzania na nchi za kigeni havitabadilika hata baada ya kuondoka madarakani Novemba, mwaka huu.
Rais Jakaya Kikwete
Kadhalika, Rais Kikwete aliwahakikishia viongozi wa nchi wanachama wa AU kuwa anaondoka madarakani, lakini Tanzania waliyoizoea na kuijua itabakia kama ilivyo na kuwaomba viongozi hao kumpa ushirikiano mkubwa mrithi wake kama walivyompa yeye.

Rais Kikwete alitoa uhakikisho huo mara mbili, juzi wakati alipohutubia kuwaaga wakuu wenzake wa nchi wanachama wa AU wakati wa Mkutano wa 25 wa Umoja huo uliofunguliwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Sandton Convention mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Wakati wa mkutano ujao wa kawaida wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, Januari, mwakani, Tanzania itakuwa na Rais mpya.

Alirudia kauli na msimamo huo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Somalia, Hassan Sheikh Mahmoud, na kiongozi wa Somalia alimjulisha Rais Kikwete kuwa angependa kutembelea Tanzania baadaye mwaka huu.

Alisema Rais Kikwete alisema misingi ya siasa za nchi za nje za Tanzania na misingi mikuu ya kuongoza mahusiano yake na nchi za nje yaliwekwa tangu uhuru na hasa tangu kutungwa wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania mwaka 1972 na tangu wakati huo haijapata kubadilika hata kama wamebadilika viongozi mara nne sasa.

“Hatujapata kubadilisha misingi hiyo inayoelekeza kuwa mahusiano yatajengwa kuanzia nchi za jirani, zikifuatiwa na nchi za Afrika, nchi marafiki duniani na nchi nyinginezo,” alisema.

Wakati huo huo, Rais Kikwete ameelezea mambo makubwa saba ambayo Tanzania iliyasimamia kwa kusaidiana na nchi nyingine ama kuyaongoza katika miaka 10 wakati wa utawa wake.

Alitaja mambo hayo kuwa akiwa Mwenyekiti wa AU, alisimamia uanzishwaji wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Afrika na nchi za India, Uturuki na Umoja wa Ulaya 

Jambo jingine ni kuongoza Operesheni ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika kilichomwondoa madarakani Muasi Kanali Mohamed Bakar katika Kisiwa cha Anjouan na hivyo kulinda uhuru na umoja wa Visiwa vya Comoro.

Rais Kikwete pia alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za AU kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi (2012-2014), Tanzania iliwezesha kubuniwa na kuliwezesha Bara na msimamo kuhusu tabia nchi na mpango wa kuutekeleza – Climate Change Concept Paper and Climate Change Action Plan.
 Chanzo Nipashe
 
Top