Baraza la taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) limekifungia kiwanda cha Huwa Cheng Company limited kilichopo mjini Dodoma na kutoza faini ya shilingi milioni 200 baada ya kubaini kiwanda hicho kinajihusisha na usindikaji wa nyama ya Punda kinyume na utamaduni wa watanzania huku mazingira yake yakiwa hatarishi kutokana na uchafu unaozalishwa kuzagaa kwenye makazi ya watu.
Ni mabishano makali baina ya
wamiliki wa kiwanda hiki raia wa uchina na maofisa wa NEMC yaliyochukua muda
mrefu kabla ya maofisa hao kutoa tamko la kufungwa kwa kiwanda hicho ambacho
mbali na kuzalisha nyama ya Punda ambayo ni kinyume na utamaduni wa watanzania
lakini pia mazingira ya uzalishaji wake ni hatarishi kwa afya za wafanyakazi na
majirani wa eneo hilo.
Kiwanda hiki ambacho kwa siku
kinadaiwa kuchinja Punda wasiopungua 200 inaelezwa kuwa mbali na kukiuka
utamaduni lakini pia kinaharibu kizazi cha wanyama hao ambao uzao wake unatajwa
kuwa ni mdogo hali inayotishia wanyama hao ambao kwa kanda ya kati hutumiwa
katika kazi mbalimbali kupungua ama kutoweka kabisa.
Mohamed Hamis ni meneja msaidizi
wa kiwanda hiki ambaye anazungumza kwa niaba ya raia hao wa uchina anasema
nyama hizo za Punda zinasafirishwa kwenda kuuzwa nchini China.
Sintofamahu hii inakifanya Chanzo chetu kuzungumza na wakazi wa mji wa Dodoma ambao wanatupa lawama kwa mamlaka za mkoa
kutobaini kiwanda hicho na kukichukulia hatua huku kukiwa na taarifa ya nyama
hizo kuzagaa na kuuzwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo hasa kwenye mabaa na
migahawa ya chakula.
Chanzo ITV