Kundi la wananchi leo limevamia ofisi ya serikali ya kata ya Njoro, manispaa ya Moshi, na kuichoma moto wakipinga matokeo yaliyompa ushindi mgombea wa Chadema, Jomba Kayi.
Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa katika magari matano,
walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao na pia
kufanikiwa kuwakamata wananchi 106 kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya wananchi hao
walionekana wakishangilia kwa kupeperusha bendera za CCM na vitambaa vyenye
rangi ya njano na kijani wakati wakipelekwa polisi.
Katika uchaguzi huo, Koyi aliibuka mshindi kwa kupata kura 3,181
akifuatiwa na mgombea wa CCM, Zuberi Kidumo aliyepata kura 2,467 na Hamad Nkya
wa ACT-Wazalendo aliyepata kura 106.
Polisi wa FFU na Askari kanzu, walionekana wakipita barabara
mbalimbali za mji wa Moshi kuelekea kituo cha kati cha Polisi wakiwa na
watuhumiwa hao huku magari yao yakihanikizwa na ving’ora.
Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani
alilithibitishia gazeti hili kuchomwa kwa ofisiu hiyo na kufafanua kuwa Jeshi
lake limewatia mbaroni wananchi 106 kuhusiana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa Ngonyani, tukio hilo lilitokea kati ya saa 4:00 na
saa 5:00 asubuhi baada ya wananchi hao kuandamana na kwenda kuchoma ofisi hiyo
wakipinga ushindi wa mgombea wa Chadema,Koyi.
Kamanda Ngonyani alisema polisi walilazimika kutumia nguvu ikiwamo
kupiga mabomu ya machozi baada ya wananchi hao kuanza kuwarushia mawe polisi
waliokwenda eneo hilo kudhibiti vurugu.
“Nataka niwatahadharisha wananchi kuwa polisi tuko imara na yeyote
anayetaka kuvuruga amani tutamchukulia hatua za kisheria bila kujali ni mfuasi
wa chama gani au kiongozi wa kisiasa,”alisema.
Koyi alipoulizwa jana aliwalaumu polisi kwa kile alichodai kulea
uovu wa baadhi ya wafuasi wa CCM ambao walianza kujichukulia sheria mkono hata
kabla ya yeye kutangazwa mshindi wa Udiwani.
“Hayo ni matokeo ya polisi wenyewe kuwalea. Walivunja ofisi
wakaiba sanduku la kura za Urais hawakuchukuliwa hatua. Wakapiga wasimamizi
polisi wakaa kimya na sasa wamechoma ofisi,”alidai.
Koyi alidai taarifa za uovu wa wafuasi hao ziko polisi lakini
hawakuchukuliwa hatua, akisema zipo njia za kisheria za kupinga matokeo ya
uchaguzi kama hukuridhika badala ya kuchukua sheria mkononi.
Miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo, Ramadhani Juma na Kasim Ali,
walidai wananchi hao waliamua kuchoma ofisi hiyo kupinga utaratibu uliotumika
kumtangaza Koyi kuwa mshindi.
“Utaratibu ni kwamba msimamizi alitakiwa atangaze matokeo lakini
yeye akamtangaza mshindi tu bila kuainisha idadi ya kura wala kubandika matokeo
hayo. Hii ndio tatizo lilipoanzia,”alidai Juma.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Moshi mjini, Joel Makwaia, alidai
mgombea wa CCM ndiye aliyeshinda katika uchaguzi huo lakini zikafanyika hujuma
na kumtangaza Koyi ndiye mshindi.
Makwaia alisema kuna baadhi ya masanduku ya kura ya Rais yaliibwa
na baadae kuonekana mitaani hali ambayo iliibua hasira kutoka kwa wananchi hao
wakihisi matokeo yalichakachuliwa.
Kiongozi huyo alitetea hatua ya watu waliochoma ofisi hiyo
kukimbilia ofisi za CCM kata ya Njoro, akisema walifanya hivyo kwa vile
wanaimani CCM kitawasaidia kupata haki yao wanayoidai.
“Niombe Mamlaka husika iweze kuingilia kati katika kata hii ya
Njoro. Uchaguzi huu umewanyima haki wananchi wa kata ya Njoro wakaamua kuchoma
ofisi kutokana na kutotendewa haki,”alidai.
Ofisa uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Ramadhan
Hamisi alipoulizwa juu ya sakata hilo alielekeza atafutwe msimamizi wa
uchaguzi, Jeshi Lupembe ambaye hata hivyo hakupatikana.
Katibu Muhtasi wa msimamizi huyo aliyepokea simu alisema bosi wake
alikuwa nje ya ofisi na alikuwa hajui angerejea muda gani. Hadi tunakwenda
mitamboni alikuwa bado hajapatikana.
CHANZO: MWANANCHI